Habari Mseto

Mama Jowie azirai kortini baada ya kilio mwanawe aliporudishwa ndani

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KILIO kilipasua kimya ndani ya mahakama pale mshukiwa wa mauaji aliyeelezewa na mahakama kuwa “mlaji wa wanawake” ama “chagundoa” aliponyimwa dhamana na kuamriwa akae ndani hadi Juni 18, 2019 kesi ya mauaji inayomkabili itapakaposikizwa.

Mama yake Joseph Irungu almaarufu Jowie alizirai mahakamani na kusaidiwa kusimama na askari jela,  mwanawe aliponyimwa dhamana na mpenziwe Jacque Maribe kuachiliwa huru.

Mama yake Irungu alipiga duru “woooi wooi woooi” kisha akaanguka huku dada zake Maribe na mama yake wakitetemeka.

Marafiki wa Maribe na watu wa familia yake walikuwa wanajishika tama Jaji James Wakiaga alipokuwa anasoma uamuzi wa dhamana.

Jasho liliwatoka marafiki wa Maribe huku wakishikilia pumzi muda wote Jaji Wakiaga alipokuwa anasoma uamuzi wa dhamana.

Hata Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria alionekana mwenye wasiwasi sawia na mkurugenzi wa masuala ya dijitali wa Ikulu Dennis Itumbi.

Jaji Wakiaga alisababisha wengi kupatwa na huzuni aliposema  “Irungu hana kazi maalum. Yeye hufugwa na wanawake anaowachumbia katika nyumba zao. Yeye ni mfano wa kiume wa “slay queen”, chagundoa, ama “mla wanawake” asiye na kazi maalum na huishi maisha ya raha mustarehe.”

Jaji alisema kati ya 2012 na 2017 alikuwa akifanya kazi Dubai na 2017 akawa anawalinda wanasiasa nyakati za kampeini kwa vile yuko na ujuzi wa kutumia bastola.

Jaji alisema mshtakiwa huyu atarokea mataifa ya Uarabuni akiachiliwa kwa dhamana.

Alisema yeye ni tisho kwa mashahidi ikitiliwa maani ni mtaalam wa kutumia bastola, atahakikisha kuwa mashahidi walioorodheshwa kutoa ushahidi.

Na wakati huo huo Jaji James Wakiaga alifanya mzaha na msimamo wa Maribe kuwa “ anaweza kupatikana na hatia ya mapenzi tu anayompenda Irungu.”

Jaji alisema hakuna makosa kama hayo katika sheria za Kenya lakini akasema wapenzi hufanya vituko na mambo ya kishenzi katika jina la upendo.

Akasema , “Nimeambiwa na Biblia Takatifu kuwa Adamu alimkosea Mungu kwa kula tunda lililokatazwa kwa vile alitaka kumpendeza mkewe Awa. Alikula itimie neno ‘ikiwa ni kufa tufe pamoja’.”

Jaji Wakiaga alisema wapenzi huua ili kufurahishana.