Habari Mseto

Wateja wa Multichoice na DSTV kupata burudani zaidi Krismasi

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

KAMPUNI za Multichoice na DSTV zimezindua mpango maalum wa kuwaburudisha wateja wake msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zinapokaribia.

Mpango huo unahusisha kuanzishwa chaneli tano maalum za televisheni, zitakazokidhi mahitaji ya wateja wake kama watoto, wapenzi wa kandanda, wapenzi wa sinema za Afrika Mashariki na familia nzima kwa jumla.

Meneja Mkuu wa Multichoice nchini, Bw Eric Odipo, alisema mpango huo unalenga kuimarisha mahitaji ya wateja wao, ambao wengi watakuwa nyumbani msimu huu wa sherehe.

Baadhi ya chaneli zitakazozinduliwa ni East African Movie Fest, itakayopeperusha sinema za Kenya, Tanzania na Uganda.

“Tunalenga kuhakikisha kuwa kila mmoja amenufaika kutokana na huduma za burudani tunazotoa,” akasema Bw Odipo.

Ili kupata huduma hizo, mteja atahitajika kuwasilisha king’amuzi chake kwa wahudumu wa kampuni hizo ili kuwezeshwa kupata huduma hizo.

“Muhimu ni kuwa wateja hawatatozwa ada zozote mbadala kupata huduma hizo. Lengo ni kuhakikisha kuwa tumewapa burudani ya kutosha,” akasema Bw Odipo.

Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Kikanda wa DSTV Sharleen Samat alisema kuwa mkakati huu ni mwanzo tu wa ushirikiano ambao lengo lake ni kupanua zaidi soko lao, ili kuwafikia wateja wengi zaidi katika siku za usoni.

“Ingawa tu washindani katika utoaji huduma za televisheni, lengo moja kuu ni kuhakikisha kuwa tumedumisha ubora wa huduma tunazotoa,” akasema.