TAHARIRI: Usalama wa raia upewe kipaumbele
NA MHARIRI
Tukio la kilipuzi kutupwa katika makao ya watoto eneo la Burat, Kaunti ya Isiolo juzi na kuua mtoto mmoja, wengine wanane wakijeruhiwa ni la kuvunja moyo sana.
Isitoshe, takriban wezi 200 wa mifugo walivamia kijiji cha Nadome katika Kaunti ya Baringo wakaiba ngómbe 700 na kumteka nyara msichana wa umri wa miaka 12.
Kuna mambo mengi zaidi tunayosherehekea humu nchini, lakini suala la usalama wa raia, hasa katika maeneo yenye wizi wa mifugo, si miongoni mwayo.
Matukio ya wizi wa mifugo na uharibifu wayo ni yale yale kila mwaka. Ni suala ambalo halijapata ufumbuzi na suluhu ya kudumu.
Kundi la watu 200 kuvamia kijiji na kuiba mifugo 700 si jambo linalofaa kufichwa na si shughuli inayoanza na kuisha kwa muda wa dakika chache.
Kulingana na kiwango cha juu cha ujasusi katika kikosi chetu cha polisi, na mageuzi makubwa katika idara ya polisi yaliyofanywa hivi majuzi, inashangaza jinsi tukio la Nadome lilitokea bila ya polisi kujua na kupambana na wahalifu hao ili kuzuia wizi huo.
La kuhuzunisha ni kwambamatukio kama haya yamekuwa ya kawaida. Ujumbe wa polisi wa ngazi ya juu na pengine wakiandamana na Waziri wa Usalama wa Ndani Bw Matiang’i wataenda Nadome kutoa taarifa za namna ya kukabiliana na uhalifu huo, kisha yaishie hapo.
Serikali imewekeza pakubwa katika idara hii na raia wanahitaji kuona natija ya utendakazi wao.
Uzinduzi wa mamia ya magari ya polisi mwaka jana ulilenga kuboresha kazi yao ya kukabili wahalifu na uhalifu. Hapajawa na natija kubwa hata baada ya Waziri Matiang’i kuzindua magari mengine majuzi.
Hatujasahau mauaji ya Suguta Valley mwaka 2012 na Kapedo, 2014 ambapo polisi 63 waliuawa kinyama.
Kupelekwa kwa wanajeshi Kapedo mwaka 2014 Kapedo hakukuleta tofauti yoyote.
Hivyo basi, usalama wa Wakenya unapaswa kipaumbele na serikali yoyote ile. Ni sharti Wakenya walindwe dhidi ya uchakaramu huu iwapo tunataka kushuhudia maendeleo na kuboreka kwa uchumi wa nchi.