Wazazi wa watahiniwa waliojifungua kukamatwa
NICHOLAS KOMU, WANDERI KAMAU na FAITH NYAMAI
WAZAZI wa watahiniwa ambao walijifungua wakati wa mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) watakamatwa, Katibu wa Wizara ya Elimu Bellio Kipsang alisema Alhamisi.
Alisema wazazi hao watakabiliwa kwa kuwalinda wahusika wakuu dhidi ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hii ni kufuatia visa vingi vya wanafunzi kujifungua wakati wa mtihani huo ambao ulianza Jumanne na kukamilika jana.
Hata hivyo Dkt Kipsang hakueleza jinsi wazazi wanavyohusika katika mimba za watoto wao wachanga na sheria itakayotumika kuwakamata ama kuwashtaki.
“Mojawapo ya masuala makuu ambayo yamejitokeza katika mtihani wa mwaka huu ni idadi kubwa ya wanafunzi waliojifungua. Hao ni watoto wadogo. Hilo ni sawa na dhuluma za kimapenzi,” akasema Dkt Kipsang katika Kaunti ya Nyeri baada ya kushuhudia usambazaji wa karatasi za mtihani huo.
Kufikia jana, watahiniwa kutoka pande nyingi za nchi walikuwa wameripotiwa kujifungua tangu mtihani huo kuanza.
Waziri wa Elimu Amina Mohamed pia alilalamikia visa hivyo, akisema kuwa wizara tayari imeanza mikakati ya kufahamu kiini cha visa hivyo.
Kwenye kikao na wanahabari katika Gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi, waziri alisema alikuwa amepokea visa tisa vya wasichana waliojifungua na akaahidi uchunguzi zaidi.
“Tungali tunaendelea na uchunguzi wetu kuhusu visa hivyo. Hata hivyo, inasikitisha kwamba kiwango cha matineja wanaopata mimba kabla ya muda ufaao kinazidi kuongezeka. Ni hali ambayo lazima tuishughulikie kwa dharura,” akasema.
Kama hatua ya kukabili visa hivyo, waziri aliagiza maafisa wa ubora katika wizara hiyo kuandaa ripoti kamili kuhusu sababu zinazopelekea kuongezeka kwa visa hivyo.
Baadhi ya kaunti ambazo visa hivyo viliripotiwa ni Kwale, Mombasa, Kitui, Nyandarua, Embu kati ya zingine.
Waziri aliwarai wazazi kuwalinda watoto wao dhidi ya kushiriki ngono mapema, kwani hilo linaathiri sana mustakabali wao.