• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mzee Moi amuita Kalonzo kwa mazungumzo

Mzee Moi amuita Kalonzo kwa mazungumzo

Na MWANDISHI WETU

RAIS Mustaafu Daniel Moi sasa amemwalika aliyekuwa makamu wa Rais na pia kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kumtembelea nyumbani kwake Kabarak, kwa mazungumzo.

Mzee Moi, ambaye amekuwa akiugua alimtuma mwanawe, seneta wa Baringo Gideon Moi kufikisha ujumbe wa mwaliko wake kwa Bw Musyoka Alhamisi, wakati seneta huyo alifika nyumbani kwa Bw Musyoka kupeleka risala za rambirambi kutokana na kifo cha babaye Kalonzo, Mzee Peter Musyoka.

Wakati wa ziara hiyo ya nyumbani kwa Kalonzo mtaani Karen, Jijini Nairobi, Bw Moi alisema Mzee Moi ana haja ya kumwona Bw Musyoka ili kumpa pole zake moja kwa moja, akiongeza kuwa marehemu Mzee Musyoka alikuwa rafiki ya Mzee Moi.

“Pole sana kutoka kwangu, familia yangu, watu wa Baringo, chama chetu na zaidi kutoka kwa Mzee. Mzee asingeweza kuja kutokana na changamoto kidogo lakini amesihi wakati utakapojihisi mwenye nguvu uende umwone na akupe pole zake binafsi,” akasema Bw Moi, ambaye pia ni mwenyekiti wa KANU.

Bw Musyoka bila kusita alipokea mwaliko huo, akiahidi kuwa “tutakuja sisi sote.”

“Hata tunadhani kuwa hii ingefanyika kitambo sana na tunataka kuja haraka tuwezavyo,” akasema Kalonzo, ambaye alieleza kuwa babaye atazikwa Ijumaa wiki ijayo.

“Tunaheshimu mzee, ni rika moja na mzee wetu na walijuana tangu zamani,” Bw Moi akasema.

Bw Musyoka sasa atakuwa kiongozi wa tano wa hadhi ya juu kumtembelea Mzee Moi nyumbani kwake kwa ziara rasmi, baada ya Rais Uhuru Kenyatta, Mjumbe Maalum wa AU na pia kiongozi wa ODM Raila Odinga, Katibu Mkuu wa muungano wa wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli na Gavana Ali Hassan Joho.

Hata hivyo, Naibu wa Rais William Ruto licha ya kuonyesha ari ya kutaka kukutana na Mzee Moi miezi michache iliyopita hakufanikiwa, kwani wakati mmoja alienda hadi Kabarak lakini akakosa kukutana naye.

Wandani wa Bw Ruto baadaye walimlaumu seneta wa Baringo kuwa alikuwa kizingiti kwa Bw Ruto kukutana na mzee.

Ziara za viongozi hao nyumbani kwa Mzee Moi zimekuwa zikitafsiriwa kisiasa kuwa huenda zina mkono katika uchaguzi ujao wa 2022.

Haya yanajiri wakati mjadala unaendelea kuhusu hatima ya kisiasa ya Rais Uhuru Kenyatta baada ya kustaafu ifikiapo 2022.

Jana, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli alirejelea wito wake kuwa Rais Kenyatta awe Waziri Mkuu awamu yake ya Urais itakapokamilika 2022, akizidi kupigia debe katiba ifanyiwe marekebisho.

Bw Atwoli amesema kuwa katiba ikirekebishwa kutakuwa na nafasi za kutosha kwa uwakilishi wa jamii tofauti, akisema kuwa Rais Kenyatta bado ndiye mwakilishi thabiti wa jamii ya Mlima Kenya na hafai kustaafu.Bw Atwoli alisema kuwa kufanywa kwa kura ya maamuzi ya kurekebisha katiba ni uamuzi ambao Wakenya hawana budi ili kuufanya, ili changamoto haswa za ukosefu wa uwakilishi wa baadhi ya jamii ambazo zimekuwepo zisuluhishwe.

“Wazo langu halikuwa lisilo la kawaida kwani tukipanua serikali na kuunda kiti cha Waziri Mkuu kulingana na maelewano ya Bomas Draft, Wakenya wanaweza kusema kiti hicho kikaliwe na mtu kutoka eneo la Mlima Kenya na Rais Kenyatta akiwa ndiye kiongozi mkuu zaidi eneo hilo na ambaye wakati huo atakuwa amekamilisha awamu yake anaweza kushauriwa achukue nafasi hiyo kama chaguo la eneo hilo,” akasema Bw Atwoli, kupitia ujumbe.

“Na hiyo itakuwa hivyo kwa kiti cha Urais na wengine na hii ndiyo njia bora zaidi ya kumpa kila Mkenya imani ya kuwa sehemu ya serikali mpya.”

Lakini Bw Atwoli alisema Rais Kenyatta awache kusumbuliwa kwa sasa kwani anashughulika na kazi ya kutimiza ajenda zake nne kuu za maendeleo, kinyume na naibu wake William Ruto ambaye kazi yake ni kuzunguka akipiga siasa.

“Tayari Rais Kenyatta ana kazi nyingi, kinyume na naibu wake ambaye tayari ameeleza azma yake ya 2022 na anafikia kila Mkenya nchini kote kutafuta uungwaji mkono,” akasema.

You can share this post!

KUTULIZA JOTO: Uhuru ampeleka Raila kwa Ruto

Sh2 bilioni za upanzi wa miti zatoweka

adminleo