Habari Mseto

Mholanzi kizimbani kwa kulawiti watoto, wakili amhepa kortini

November 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Uholanzi alifikishwa mahakamani Ijumaa kujibu mashtaka ya kuwabaka wasichana wa umri mdogo aliokuwa anafadhili elimu yao.

Bw Hans Egon Dieter, wakili aliyestaafu mwenye umri wa miaka 66 alikana mashtaka mawili ya kuwabaka na kuwalawiti wasichana wenye umri wa miaka minane na kumi katika makazi yake mtaa wa Roysambu Nairobi miaka minne iliyopita.

Raia huyo wa kigeni mwenye mazoea ya kuwadhulumu wasichana kimapenzi aliamriwa azuiliwe gerezani hadi Novemba 16 mwaka huu wakati walalamishi watakapofika mahakamani kutoa ushahidi.

Bw Dieter alipata mshtuko wa mwaka baada ya wakili aliyekuwa amesikizana naye amtetee Bw David Ayuo kutoweka mahakamani.

Ilibidi mshtakiwa ajikakamue na kujieleza.

Bw Hans akiwa kizimbani akisemewa mashtaka. Picha/ Richard Munguti

“Tumekuwa na wakili David Ayuo hapa kortini. Naomba korti isitishe kesi yangu kumsubiri Bw Ayuo. Huenda ameenda kujisadia, atarudi,” Bw Dieter alimweleza hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Caroline Muthoni Nzibe.

Mahakama iliahirisha kesi yake hadi saa saba mchana kumpa muda wakili Ayuo kurudi, lakini wapi!

Ilibidi hakimu amweleze mshtakiwa ajitetee na kujibu madai ya kiongozi wa mashtaka Bi Edna Ntabo.

Bi Ntabo alipinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana akisema “ kwa muda wa miaka miwili alikuwa ametoroka.”

Pia alisema mshtakiwa atawavuruga mashahidi kwa vile wengi wao ni wale huwasaidia katika shule yake ya kibinafsi iliyoko eneo la Kiusyani , kaunti ya Kitui.

Bali na kuwabaka wasichana hao mshtakiwa alikuwa akiwapiga picha akiwatendea unyama huo wa kuwabaka.

Picha hizo, idara ya kutetea haki za watoto katika afisi ya mkurugenzi wa jinai , ilisema alikuwa anazipeperusha katika mitandao mbali mbali na kujizolea fedha kutokana na dhuluma hiyo.

Mzongo wa mawazo wamtafuna kortini. Picha/ Rivhard Munguti

Bw Dieter, kutoka Netherlands, alikuwa akiandamwa na idara hiyo ya kushughulikia haki za watoto tangu mwaka wa 2016 hadi Oktoba 1 , 2018 alipotiwa baroni baada ya kukwepa mitego ya polisi kwa muda wa miaka minne.

Akipinga kuachiliwa kwa dhamana, Bi Ntabo alisema mshtakiwa atatoroka na kupotelea Netherlands.

Mshtakiwa alipinga alikuwa ametoroka akisema alikuwa ameugua na kulazwa hospitali miezi minne kaunti ya Mombasa.

“Nimeoa hapa nchini. Mimi na mke wangu tunaishi eneo la Kiusyani kaunti ya Kitui. Mke wangu anaitwa Rachel. Ndoa yetu imebarikiwa na mtoto mmoja , msichana. Hata nikiachiliwa kwa dhamana nitaenda kuishi Kiusyani, kaunti ya Kitui,” alisema Bw Dieter.

Raia huyo wa kigeni alisema alikuwa na kesi nyingine sawa na ya sasa inayomkabili na kuwa yuko nje kwa dhamana.

“Niko na cheti cha dhamana katika kesi hiyo nyingine. Niko na cheti cha dhamana. Nitawasilisha uthibitisho kuonyesha niko nje kwa dhamana na pia nyingine kuthibitisha nilikuwa nimelezwa hospitali,” alisema Bw Dieter.