Dondoo

Madereva wasimulia kukutana na jini jike

November 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VICTORIA NDUVA

Kyumbi, Machakos

Madereva wanaotumia barabara kuu ya Nairobi kwenda Mombasa wanataka viongozi wa kanisa kuwaokoa kutokana na jinamizi la mazingaombwe wanayodai yanahatarisha maisha ya wengi eneo hili.

Kulingana na mdokezi ambaye ni dereva wa lori, wanapofika eneo hili usiku wa manane huwa wanashuhudia kioja cha mwanamke mrembo anayesimamisha gari.

Alidai kwamba mwanamke huyo huwa mrembo wa ajabu kiasi kwamba madereva hulazimika kusimamisha magari yao kumsikiliza.

Kulingana na mdokezi, dereva akikataa kusimamisha gari huwa anakumbana na mkosi mkubwa na hafanikishi shughuli zake za siku hiyo.

Inasemekana kuwa wakati mwingine, mwanamke huyo hubadilika kuwa chatu mkubwa ambaye huvuka barabara kwa mwendo wa kinyonga jambo ambalo huwafanya madereva kusimamisha magari barabarani ili kumpisha.

“Unamuona mwanamke upande mmoja wa barabara akisimamisha gari, ghafla bin vuu, anageuka chatu na kuanza kuvuka barabara na unasimamisha gari kwa mwendo wa hata saa moja,” alisema mdokezi.

Dereva mmoja alisimulia kwa machozi masaibu yake aliposimamishwa na mwanadada huyo akidhani alikuwa safarini.

Alisema baada ya dakika kumi, malkia alichukua usukani wa kuliendesha gari lile bila idhini yake.

“Sikujua kilichofanyika. Nilijipata kando huku mwanadada akidhibiti gari bila kuchoka,” alieleza. Alieleza kuwa mwanamke huyo huwaonya dhidi ya kusimulia masaibu anayowasababishia.

Kwa sasa madereva hao wanataka maombi maalum kufanywa na ikibidi wazee wafanye tambiko ili kutakasa eneo hili.

Baadhi yao wamelazimika kutumia njia mbadala ili kufanikisha shughuli zao za usafiri iwapo watalazimika kusafiri usiku. Kwa sasa hawajui kile ambacho kitawapata kwani tayari wametoboa siri ile. Wanahofia kuwa labda ghadhabu ya jini jike huyo zitakuwa juu yao.