Habari Mseto

KCSE: Ajabu ya wasichana 13,600 kupata mimba Kilifi

November 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES LWANGA

IDARA ya Watoto imetoa ripoti ya kutisha inayoonyesha kuwa wanafunzi 13,624 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 walipata mimba katika Kaunti ya Kilifi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Haya yanajiri wakati ambapo swala la mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi limezua mjadala nchini hasa baada ya watahiniwa kadhaa wa KCPE na KCSE kujifungua wakifanya mtihani.

Afisa mkuu wa masuala ya watoto Kaunti ya Kilifi, Bw George Migosi alisema eneo bunge la Kilifi Kaskazini ndilo linaloongoza likiwa na visa 3,134 likifuatiwa na Magarini na Kaloleni kisha Kilifi Kusini, Ganze na Rabai

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Migosi alisema idadi hiyo imekuwa ikipanda kila mwaka kutokana na malezi duni.

Cha kushangaza zaidi ni kuwa kuna visa 290 vya mimba za mapema vilivyoripotiwa kwa watoto wa kati ya miaka 10 na 14.

“Ripoti hii inatisha kwani tunaongea kuhusu visa 14,000 vya ndoa za mapema katika muda wa mwaka mmoja katika kaunti hii,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Migosi aliwaonya wazazi ambao hawaripoti kesi za mimba za mapema, akisema huenda wakakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuzembea katika utekelezaji wa majukumu yao ya malezi.

Mwanaharaki wa masuala ya dhuluma za kijinsia katika Kaunti ya Kilifi, Bi Helda Esliy, alisema wazazi wengi wanalaumu umaskini kama chanzo cha ongezeko la visa vya ndoa za mapema.

Kwa upande wake, kinara wa shirika la Sauti ya Wanawake, Bi Joyce Kambi aliwalaumu akina mama kwa ongezeko la visa hivyo, akisema kuwa baadhi ya akina mama hao huwapeleka mabinti zao kwa waganga ili waavye mimba.