Habari Mseto

Wazazi wawape wanao mafunzo ya dini – Polisi

November 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na HAMISI NGOWA

POLISI katika eneo la Likoni Kaunti ya Mombasa wanawashauri wazazi kutumia likizo ndefu ya Mwezi Disemba kwa kuwapeleka watoto wao katika taasisi za kidini kama vile madrassa kwa Waislamu na Sunday Schools kwa Wakristo ili waweze kufunzwa maadili mema.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo, Bw Benjamen Rotich, alisema wazazi wanafaa kutumia likizo hiyo kuhakikisha watoto wao wanapokea mafunzo ya kidini yenye muongozo mwema wa kimaisha.

Bw Rotich aidha alitoa onyo kwa watoto ambao watapatikana wakizurura au kujihusisha na visa vya uhalifu kwamba watakumbana na mkono wa sheria.

Alisema wazazi wanafaa kuchukuwa majukumu yao kwa kuwapa watoto muongozo mwema wa maisha yatakayowasaidia katika siku za usoni.

“Nawashauri wazazi kutumia hii likizo ya Disemba kuwapa vijana wao muongozo mwema wa maisha, alisema.

kwa kuwapeleka katika taasisi za kidini zinazofunza maadili mema,’’ akasema.

Polisi katika eneo hilo wamejiandaa vilivyo kukabiliana na magenge ya vijana wahalifu watakaojaribu kuvuruga hali ya usalama katika eneo hilo.

Wakati huo huo, Bw Rotich alionya wazazi dhidi ya kuwatetea vijana wahalifu wanapokamatwa na maafisa wa polisi akisema kwamba hata wao pia watatiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka.

“Kama unahuruma na mtoto wako basi chukuwa jukumu la kuhakikisha hajihusishi na uhalifu. Lakini iwapo utasikia amekamatwa kwa kujihusisha na uhalifu kisha uje utake kumtoa katika seli zetu, pia hata wawe tutakuweka ndani na kukupeleka kotini,’’ akaonya Bw Rotich.

Alisema usalama katika eneo hilo umeimarishwa mara dafu wakati huu wa likizo hii ndefu ya Mwezi Disemba ambapo idadi kubwa ya wageni wanatarajiwa kufurika katika fuo za Bahari.

Rotich aliwahakikishia wenyeji na wageni kuwa kuna maafisa maalum wa kushika doria, watakaozuia au kukabili visa vyovyote vya utovu wa usalama.