Mahitaji ya visa kwa Wakenya Afrika Kusini yalegezwa
Na BERNARDINE MUTANU
Serikali ya Afrika Kusini imewaondolea Wakenya vikwazo vya kuingia nchini humo.
Hii ni baada ya serikali hiyo kuamua kuwapa Wakenya wanaozuru nchini humo kwa biashara au masomo visa tofauti zitakazodumu kwa miaka 10.
Wakenya ambao hufanya ziara za kila mara watapewa viza aina tofauti zitakazodumu kwa miaka mitatu kuanzia Desemba 1.
Hii ni baada ya majadiliano na makubaliano kati ya Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na mwenzake wa Afrika Kusini Malusi Gigaba Jijini Pretoria mapema Jumatatu.
Maafisa wa serikali wanaozuru nchini humo watapewa visa inayodumu miezi mitatu bila malipo yoyote mara moja, kulingana na tangazo kutoka Wizara ya Usalama wa Ndani.
Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo baada ya Kenya kulegeza mahitaji yake ya viza kwa raia wote kutoka Barani Afrika kwa lengo la kukuza ushirika miongoni mwa mataifa ya Afrika.