Sakaja aorodhesha sababu za moto kutokea Gikomba kila mara
Na CHARLES WASONGA
MIZOZO ya ardhi, ukosefu wa bima na hali ya wafanyabiashara kuhujumiana kila mara ni baadhi ya sababu ambazo huchangia kutokea kwa mikasa ya moto kila mara katika soko la Gikomba Nairobi.
Hii ni kwa mujibu wa Seneta wa kaunti hiyo Johnson Sakaja ambaye pia alilaumu idara ya kuzima moto akiilamu kwa kushindwa kudhibiti moto haraka kabla ya hasara kupatikana.
“Kwa kuwa soko la Gikomba liko katika ardhi ya umma kumekuwa na vuta nikuvute nyingi kwa sababu kuna watu ambao wanataka kunyakua ardhi hiyo ili wajifaidi wao wenyewe,” akasema huku akiitaka serikali ya kaunti ya Nairobi kuingilia kati suala hilo.
Bw Sakaja alisema hayo Jumatano asubuhi alipokuwa akihojiwa na wanahabari, saa chache baada ya moto huyo kutokea.
“Hii shida ambayo inawakumba wafanyabiashara hawa itakoma tu pale serikali ya kaunti ya Nairobi, Tume ya Ardhi na Serikali Kuu zitaingilia kati suala hili na kuhakikisha kuwa ardhi hii inakuwa mali ya wafanyabiasha hao. Hii ni kwa sababu wamefanya biashara kwa miaka mingi zaidi,” Bw Sakaja akaeleza.
Alisema licha ya kaunti ya Nairobi kuandaa bajeti ya Sh32 bilioni kila mwaka idara hiyo haijaweza kupewa ufadhuli wa kutosha ili iweze kushughulikia mikasa ya moto kwa dharura.
“Inasikitisha kwamba wafanyabiashara wa soko la Gikomba wamekuwa wakipata hasara kila mara ilhali kuna idara ya zima moto ambayo inafaa kudhibiti mikasa kama hiyo,” Bw Sakaja akasema.
Mali ya thamani mkubwa iliharibika katika mkasa wa jana, japo hakuna aliyefariki wale kujeruhiwa.
Inasemekana kuwa moto huo ulizuka katika sehemu ambako mbao huuzwa mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Jamatano.
Mkasa huo umetokea miezi mitano baada ya mkasa mwingi sawa na huo kutokea naktika soko hilo ambapo watu 16 walifariki na wengine kujeruhiwa mnamo Juni 20, 2018.
Baada ya mkasa huo Rais Uhuru Kenyatta, alimuru uchunguzi ufanywe ili kubaini chanzo cha mioto hiyo ya kila mara, kisha hatua zifaa zichukuliwe kuidhibiti.