• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
Harusi iliyotibuka Nakuru: Wachumba wafunguka kuhusu ukweli wa mambo

Harusi iliyotibuka Nakuru: Wachumba wafunguka kuhusu ukweli wa mambo

Na EVELYNE MUSAMBI

MWANAMUME ambaye harusi yake ilifutiliwa mbali dakika ya mwisho na pasta wake, amedai kuwa pasta na waumini wa kanisa walikuwa wakimchukia mchumba wake.

Bw Paul Waithaka alisema alikuwa ameona dalili ambazo alipuuza na ambazo anaamini zilisababisha harusi yake kutibuka dakika za mwisho.

Bw Waithaka na Joyce Wanjiru walikuwa wamepanga kufunga pingu za maisha Jumamosi iliyopita lakini Pasta Jesse Karanja alikataa kuongoza harusi yao akidai hawakuwa wametimiza masharti ya kanisa ya kukaguliwa hali ya afya zao.

Kulingana na Bw Waithaka, ambaye ni mwalimu wa shule ya upili na mkalimani katika kanisa la Mizpah House of Prayer, Kaunti ya Nakuru, harusi hiyo ilitibuka kwa sababu washirika wa kanisa walikuwa wakimchukia mchumba wake.

Alisema hakushughulika kutatua suala hilo kwa sababu hakuamini lingekuwa sababu ya kuvuruga uhusiano wake na mchungaji.

“Tulipigana vita kutoka mwanzo na kanisa la Mizpah na hii ndio sababu hatukufanyia hafla ya kuandaa harusi kanisani humo. Joyce hakukubaliwa kutoka siku ya kwanza walipojua tulipanga kuoana na sikujua vita hivyo vingefikia hapo. Lakini ninaamini kuna sababu ya mambo kuwa yalivyokwenda,” alisema.

Wawili hao waliandaa hafla mbili za kukusanya pesa za harusi yao, ya kwanza ikifanyika Nairobi ambapo Bi Wanjiru hufanya kazi na ilihudhuriwa na marafiki na washiriki wa kanisa. Ya pili iliandaliwa Njoro ambapo wazazi wa Waithaka wanaishi.

Wawili hao hawajazungumza na Pasta Karanja tangu kisanga cha kuaibisha katika kanisa lake Jumamosi na hakuna afisa wa kanisa aliyewasiliana nao.

“Sijazungumza na mtu wa Mungu kwa sababu hata yeye alipitia mengi baada ya Wakenya kuanza kumtusi. Unaona, Wakenya wanapasa kufahamu kwamba hawafai kutusi watu licha ya wanachotenda.

Ni kweli tulikasirika lakini hiyo haimaanishi tumtusi. Hata hivyo, tumekuwa tukizungumza na mapasta wengine wanaotushauri na kutuombea,” alisema Bw Waithaka.

Alisema alikuwa akimwamini pasta huyo na kwamba kukataliwa kwa harusi yake kulimuumiza yeye na mpenzi wake.

“Tulijiuliza mbona sisi na kwa nini Mungu alikubali haya yatupate lakini sasa tumepiga moyo konde kwa sababu Mungu amekuwa mwema kwetu,” alisema.

“Hatuna nia ya kushtaki yeyote. Baadhi ya mambo huachiwa Mungu ambaye ndiye hutoa haki ya kweli.”

Alisema wamefaulu kulipa madeni yote waliyoweka kutokana na harusi iliyotibuka.“Tulilazimika kulipa kila mtu kwa sababu hatukutaka kusikia watu wakilalamika kwamba tulishindwa kulipa madeni ya wale waliokodisha kutoa huduma katika harusi yetu,” alisema.

“Tulikuwa na pesa zetu tulizoweka akiba na tulizochangiwa na marafiki kwenye hafla zetu Njoro na Nairobi, kwa hivyo baada ya kulipa madeni yote, tulibaki bila kitu,” alisema. Bw Waithaka alisema wazazi wa pande zote mbili wamesimama nao na wanawashauri kupanga harusi nyingine.

You can share this post!

RUTO ARUDI NYANZA TENA

Ripoti yafichua maeneo wanafunzi hupata mimba

adminleo