Habari Mseto

Ripoti yafichua maeneo wanafunzi hupata mimba

November 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

TAKWIMU za serikali zinaonyesha kuwa idadi ya wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni inatisha huku baadhi ya walimu wakilaumiwa kwa kuhusika na mimba hizo.

Ripoti ya hali ya afya katika maeneo tofauti nchini (KDHS), inasema kwamba katika baadhi ya Kaunti asilimia 40 ya wasichana wanaosoma hupata mimba na kuwa katika hatari ya kuacha masomo.

Ripoti hiyo inasema wasichana wengi wanakabiliwa na hatari ya kupata mimba kabla ya kufikisha miaka 20 kumaanisha kuwa kuna uwezekano wa kukosa kumaliza kidato cha nne.

Mapema wiki hii, waziri wa elimu Amina Mohammed, aliagiza uchunguzi ufanywe kubaini chanzo cha mimba za wanafunzi, baadhi yao wa shule za msingi. Katika mitihani wa KCPE wa mwaka huu, zaidi ya wasichana 30 walijifungua na wengine zaidi ya 100 wakaufanya wakiwa na mimba.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i pia aliagiza machifu eneo la pwani kufuatilia na kuandaa ripoti kuhusu wanafunzi waliopata mimba wote katika maeneo yao.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya KDHS, Kaunti ya Narok inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojifungua ikiwa na asilimia 40 ikifuatwa na Homa Bay ambako asilimia 33 ya wasichana hupata mimba wakiwa shuleni.

umri mdogo

Stelle Kerena mhudumu wa jamii anayetunza wasichana eneo la Olposimoru Kaunti ya Narok, aliambia Taifa Leo kwamba wasichana katika kaunti hiyo wamo hatarini. “ Ni kweli, mtoto msichana katika kaunti hii anakabiliwa na hatari kubwa ikiwa ni pamoja na ya kupata mimba akiwa na umri mdogo na kusitisha masomo,” alisema.

Alihusisha hali hiyo na mila ya kuoza wasichana wakiwa na umri mdogo.

Imeibuka kuwa huenda visa vingi vya wanafunzi kutungwa mimba haviripotiwi baada ya ripoti hiyo kuonyesha kuwa ni asilimia 14 ya wasichana wanaopata mimba Kaunti ya Kitui ambapo wanafunzi 110 waliripotiwa kujifungua walipokuwa wakifanya mtihani wa mwaka huu.

Takwimu katika ripoti ya KDHS zinaonyesha kuwa Kaunti ya Pokot Magharibi ni ya tatu kwa wasichana wanaoacha shule baada ya kupata mimba ikiwa ni asilimia 29 ikifuatwa na Tana River (28) na Nyamira (28), Samburu (26). Migori, Kwale na Bomet ziliripotiwa kuwa na asilimia 24 ya wasichana wanaopata mimba wakiwa wanafunzi.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia ni asimilia 23 ya wasichana walioacha shule kwa sababu ya mimba kulingana na takwimu zilizokusanywa katika ripoti hiyo.

Inaeleza kuwa visa vichache vya wanafunzi kupata mimba viliripotiwa Kaunti za Muranga na Nyeri (asilimia 6), Embu (7), Elgeyo Marakwet (8) na Nyandarua (9).

Ripoti inafichua kwamba mmoja kati ya kila wasichana watano hupata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 20.

Kulingana na waziri Mohammed kuongezeka kwa visa hivi kunaweza kutumbukiza nchi katika mzozo mkubwa na kuhatarisha elimu ya wasichana. Akizungumza alipowaagiza maafisa wa elimu na utawala kuchunguza visa hivi katika maeneo yao, Bi Mohammed alisema kuna haja ya hatua kuchukuliwa. “ Ikiwa hali hii inaendelea kote nchini basi, nchi inaweza kuwa katika mzozo mkubwa sana,” alisema.

Ripoti ya KDHS inafanana na takwimu za Baraza la Taifa la Idadi ya Watu (NCPD), zinazoonyesha kuwa wasichana 378,397 walio na umri wa kati ya miaka 10 na 19 walihudumiwa katika vituo vya afya kote nchini wakiwa na mimba. Kulingana na Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto (Unicef), wasichana 13,894 walipachikwa mimba katika kaunti ya Kisumu pekee mwaka jana. Ripoti ya Tume ya Walimu (TSC) inaonyesha kuwa mwaka wa 2015 walimu 126 walifutwa kazi kwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao.

Ripoti zinaonyesha kuwa visa vingi hutokea maeneo ya mashambani ambako wakazi ni masikini