• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Maswali sasa yaibuka kuhusu anayemkinga daktari bandia

Maswali sasa yaibuka kuhusu anayemkinga daktari bandia

COLLINS OMULO na RICHARD MUNGUTI

MASWALI yameikuba kuhusu anayemlinda ‘daktari bandia’ James Mugo Ndichu, maarufu Mugo wa Wairimu, baada ya polisi kukosa kueleza hatua waliyofikia kumsaka.

Kinachoshangaza ni jinsi maafisa hao walivyokuwa wepesi wa kuwakamata wafanyikazi wawili katika kliniki ya mshukiwa, lakini kufikia jana jioni hakukuwa na maelezo yoyote kumhusu.

Kinachoibua maswali ni jinsi polisi, walio na mitambo ya kisasa ya kufuatilia simu, wanavyoshindwa kujua aliko mshukiwa huyo, anayetuhumiwa kuanzisha kliniki mpya hata baada ya kufunga ya awal, baada ya kukabiliwa na mashtaka ya kuwadhulumu kimapenzi wagonjwa.

Mugo amekuwa mafichoni tangu Jumatatu wakati televisheni ya NTV ilipopeperusha habari za upelelezi kuhusu Mugo kuendesha shughuli za matibabu bila kibali, kudhulumu wagonjwa pamoja na ukiukaji mwingine wa taaluma ya matibabu.

Wengi wanajiuliza jinsi polisi wameshindwa kumkamata Mugo licha ya kuwa na uwezo wa kutumia tekinolojia kujua mahala alipo katika kila pembe ya nchi.

Idara ya DCI imesema imewatuma maafisa wake maalum kumsaka mwanamume huyo.

Habari za upekuzi zilizopeperushwa katika Runinga ya NTV, zilionyeshwa kuhusu jinsi maafisa wa kaunti hiyo walivyojaribu kukagua kliniki ya Bw Mugo bila mafanikio, ingawa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa baadaye, bali aliendeleza shughuli zake haramu.

Kwingineko katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi, Victor Gathiri Kamunya almaarufu Dkt Victor na Bi Risper Auma Ogony walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku, na kushtakiwa baada ya kupatikana wakifanya kazi katika kliniki ya Bw Mugo.

Bw Kamunya, 22, ni mwanafunzi katika taasisi ya mafunzo ya matibabu (KMTC) Kaunti ya Siaya, naye Bi Ogony, 19, ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Keriri anakosoma Diploma katika taaluma ya ununuzi na usambazaji bidhaa.

Walikanusha mashtaka saba ikiwemo kutoa huduma za matibabu bila kibali na ikaagizwa wazuiliwe kwa siku saba mahakama ikisubiri ripoti kuhusu tabia zao kabla ya kuamua kama wataachiliwa kwa dhamana.

You can share this post!

Ripoti yafichua maeneo wanafunzi hupata mimba

Aliyewaua watu 12 kwa baa California apatikana amefariki

adminleo