• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Wabunge kuchunguza mimba za mapema

Wabunge kuchunguza mimba za mapema

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameanzisha uchunguzi kuhusu ongezeko la visa vya wasichana kupachikwa mimba wakiwa shule kufuatia kilio kutoka kwa umma na wadau katika sekta ya elimu.

Serikali imelaumiwa kwa kutowachukulia hatia kali wahusika wa visa hivyo vinavyopeleka wazazi kuachiwa mzigo mkubwa kuwalea watoto wanaozaliwa kando na kugharamia masomo ya wanao.

Imeripotiwa kuwa wasichana wa kati ya umri wa miaka 12 na 18 walikuwa wajawazito walipokuwa wakifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) uliokamilika majuzi. Na zaidi ya watahiniwa 20 kati yao walilazimika kufanya mtihani huo katika hospitali mbalimbali nchini baada ya kujifungua.

Wengine wanafanya mtihani unaoendelea wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) wakiwa wakiwa wajawazito au hospitalini baada ya kujifungua watoto.

Hisia za wabunge katika kero hilo la kijamii, ziliibuliwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay Gladys Wanga, ambaye anapendekeza kuwa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu ichunguze chanzo cha mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi nchini.

Pia Mbunge huyo wa ODM anaitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melley kupendekeza suluhu la kudumu kwa tatizo hilo ambali linazuia watoto wasichana kujiendeleza kimasomo.

“Mimba miongoni mwa wanafunzi wa kike imekuwa suala la kutamausha. Ni kisa cha watoto kuwazaa watoto, hali ambayo ina athari kubwa kwa jamii kwa jumla. Je, mbona tunakosa wasaa wa kuwatunza watoto wetu,” Bi Wanga akauliza Alhamisi huku akionekana kuelekeza kidole cha lawama kwa wazazi na serikali.

Kulingana na Ripoti kuhusu Uchunguzi wa Hali ya Kiafya Nchini (Kenya Demographic Health Survey) ya 2014, wasichana wengi wa umri mdogo wanaopata mimba hulazimika kuacha shule ili kuwatunza wanao.

Mwaka huu pekee, wasichana 13,624, wenye umri wa kati ya miaka 12 na 18 wameripotiwa kupata mimba wakiwa shule katika kaunti ya Kilifi pekee

Kulingana na ripoti hiyo ya KDHS, visa vya wanafunza kupata watoto viko juu zaidi katika kaunti za eneo la Nyanza, ambazo zimeandikisha kima cha asilimia 22 zikifuatwa na Rift Valley kwa asilimia 21.2 huku visa hivyo katika eneo la pwani vikiwa asilimia 21.

Hata hivyo, visa hivyo ni vichache katika kaunti za Kati mwa Kenya zilizoandisha kiwango cha asilimia 10 huku eneo la Kaskazini Mashariki likiandikisha asilimia 12.2 ya visa hivyo vya wanafunzi kupata mimba shuleni.

Kwa mujibu wa kaunti, Narok ndio iliandikisha idadi ya juu ya visa kwa kima cha asilimia 40 ikifuatwa na Homa Bay katika asilimia 33. Kaunti ya Nyamira (asilimia 28,) Samburu (asilimia 26), Migori (24), Kwale (24).

Kaunti ya Murang’a ndio yenye visa vichache kwa kima cha asilimia 6, Nyeri (asilimia 7), Embu (8), Elgeyo Marakwet (9) na Nyandarua (10).

Kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale naye alisema shida hiyo inapasa kudhibitiwa kwa sababu inawanyima wasichana nafasi ya kunawiri kimasomo na “kuvuna matunda ambayo hujiri kutokana na fanaka masomoni”.

“Tunapaswa kubuni mbinu faafu za kukabiliana na kero hilo la wasichana kushika mimba wakiwa shuleni. Ni suala ambalo lapaswa kupewa kipaumbele kwa sababu visa hivyo vinaongezeka kila uchao,” Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini akasema.

Naye Mbunge Maalum Denita Ghati alisema hilo ni suala ambalo linapasa kushughulikiwa katika ngazi ya kitaifa kwa sababu linahujumu haki ya kikatiba watoto kupata elimu ya kimsingi

“Wazazi wanafaa kusherehekea matokeo ya watoto wao katika mitahani ya kitaifa wala sio kuzaliwa kwa watoto wengine,” akaeleza Bi Ghati ambaye kabla ya kuingia bunge amekuwa akiendesha kampeni za kukamilisha na mila ya ukeketaji wasichana katika jamii yake ya Kuria.

Duniani kote, imebainika kuwa visa vya mimba za mapema miongoni mwa wasichana huchangiwa na umasikini, vurugu katika familia, wazazi kutengana, familia za mzazi mmoja, shinikizo kutoka kwa maharimu (peer pressure), tamaa, imani za kidini na dhuluma za kimapenzi.

Sababu zingine ni kama vile, uraibu wa pombe, matumizi ya mihadarati, kukosa ufahamu na athari za kimazingira

Lakini huku visa hivyo vikiendelea kuongezeka, kumeibuka mjadala kuhusu iwapo wazazi, walezi na watunzaji watoto wanapasa kuwafunza watoto waliobaleghe kuhusu masuala ya ngono, matumizi ya kinga kama vile mipira ya mapenzi ili kuzuia mimba na maradhi ya zinaa.

You can share this post!

Aliyewaua watu 12 kwa baa California apatikana amefariki

AKILIMALI: Mafunzo muhimu kwenye warsha ya kilimo na ufugaji

adminleo