• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Maswali yaibuka kuhusu kimya cha ziara za rais

Maswali yaibuka kuhusu kimya cha ziara za rais

Na WANDERI KAMAU

HUENDA ghadhabu za Wakenya kuhusu hali ya nchi ndiyo sababu kuu ambayo imepelekea ziara za nje za Rais Uhuru Kenyatta kutoangaziwa pakubwa, wameeleza wadadisi.

Hili linatokana na kutoangaziwa kwa ziara kadhaa za rais majuzi kama ilivyo kawaida, ambapo amekuwa akisafiri katika nchi za nje bila ufahamu wa wananchi, kuagwa na maafisa wakuu serikalini au kitengo chake cha mawasiliano kutuma taarifa kwa vyombo vya habari.

Tukio la juzi zaidi ni ziara ya sasa, ambapo Rais Kenyatta yumo nchini Ufaransa kuhudhuria Kongamano la Dunia kuhusu Amani.

Ingawa ziara hiyo haikuangaziwa, hasa rais alipoondoka, taarifa kutoka kwa Kitengo cha Mawasiliano cha Rais (PSCU) ilisema kuwa alisafiri Ufaransa kwa mwaliko wa mwenzake Emmanuel Macron.

“Rais Kenyatta yumo kwenye ziara nchini Ufaransa kuhudhuria Kikao cha Hali ya Amani Duniani kwa mwaliko wa Rais Macron. Wakati wa kikao hicno, rais anatarajiwa kutoa hotuba katika kikao hicho,” ikasema taarifa.

Mnamo Septemba 21, Rais Kenyatta aliondoka nchini kimya kimya kuelekea Uchina, muda mfupi baada ya kutia saini Mswada wa Fedha kuwa sheria, licha ya pingamizi kubwa kwamba utaongeza gharama ya maisha kwa mwananchi.

Baada ya ziara ya Uchina, ambako alitia saini mikataba ya kibiashara ya Sh23.9 bilioni, rais alirejea nchini mnamo Septemba 6.

Siku iliyofuata, aliondoka ghafla na kuelekea Rwanda kuhudhuria kongamano la Kilimo Endelevu. Ziara hizo hazikutangazwa kama ilivyo kawaida.

Wiki iliyopita pia alikuwa China baada ya kuondoka bila habari kwa wananchi.

Mkondo huo umezua maswali miongoni mwa wadadisi wa kisiasa, baadhi wakisema kuwa huenda Rais Kenyatta anahofia kukosolewa na umma, kwani wengi wanakabiliwa na ugumu wa kimaisha.

Kulingana na Barack Muluka ziara za Rais Kenyatta “hazijazaa matunda” kwa Wakenya, kama wengi walivyotumaini.

“Si kawaida kwa ziara za rais kuwekwa siri. Kuna hofu kwamba rais mwenyewe na washauri wake wanahofia kuwa huenda kuweka ziara hizo wazi kila mara kukawakasirisha zaidi wananchi,” asema Bw Muluka.

Kwa upande wake, Prof Macharia Munene anataja mkondo huo kama “jambo la kawaida” kwani ziara za rais zimekuwa “jambo la kawaida.”

“Si ziara zote anazofanya rais ambazo zina uzito wa kuangaziwa. Zingine ni za kawaida tu,” asema Prof Munene.

Wakenya katika mitandao ya kijamii pia wamekuwa wakionyesha ghadhabu zao kwa ziara nying za rais nje ya nchi.

, baadhi wakimrai rais “kutoomba mkopo mwingine” hasa anaposafiri nchini Uchina.

Baadhi wamekuwa wakimkosoa rais katika kurasa zake za Facebook na Twitter, hali inayotajwa kuchangia mabadiliko ya mawasiliano na kitengo chake.

“Hilo linaonyesha kwamba wengi wanaanza kufuatia kwa kina yale rais anafanya, hasa anaposafiri nje,” asema Dkt Njoki Wamae, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

You can share this post!

Wandani wa Ruto wakashifu mahasimu kutoa ushahidi mpya...

Uhuru na Ruto wanatisha watahiniwa wa KCSE – KUPPET

adminleo