Habari Mseto

Jamii yataka idhini kukeketa mabinti wao

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Kalume Kazungu

WAZEE wa jamii ya Waboni katika kaunti ya Lamu wanataka waruhusiwe kukeketa binti zao kama njia ya kukabiliana na uasherati. Wanasema mimba za mapema na kuongezeka kwa talaka kunachangiwa na wanawake wa jamii hiyo kukosa kukeketwa.

Mzee Ali Gubo, alisema jamii hiyo ilipoendeleza ukeketaji, ndoa nyingi zilidumu huku wasichana wadogo wakiepuka kushiriki ngono,wakijua fika kwamba shughuli hiyo ni ya watu wazima waliokeketwa pekee.

“Kukeketwa ni mojawapo ya tambiko zinazoashiria kwamba mtu ametoka utotoni kuingia utu uzima na anaweza kujisimamia kimaamuzi. Tangu ukeketaji ulipositishwa, ndoa zimekuwa hazisimami tena.

Wasichana wadogo pia wamekuwa wakishiriki ngono kwa wingi na kupata mimba za mapema. Waturuhusu kuendeleza tohara kwa wanawake wetu kama jamii ya Waboni,” akasema Bw Gubo.

Jamii hiyo inaamini kwamba kupashwa tohara kwa wanawake kunasaidia kupunguza uchu wa ngono hasa miongoni mwa wanawake wao, hivyo kuboresha zaidi maadili hasa kwa wale walioolewa.

Baadhi ya wanawake wa jamii hiyo waliozungumza na Taifa Leo walisema mapendekezo yao yamepitwa na wakati.

Mama Amina Abarufa alisema wale wanaodai kuna upotovu wa maadili miongoni mwa wanawake eti kwa kukosa kufanyiwa tohara, wajichunguze wamekosea wapi.

“Tohara kwa wanawake ni hatia. Ikiwa mwanamke hana maadili si kwa sababu hajapashwa tohara. Pengine waangalie malezi yake,” akasema Bi Abarufa.