Habari Mseto

Polisi wadaiwa kusafirisha abiria kwa gari lao na kuwalipisha nauli maradufu

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MAAFISA wa polisi Jumatatu waliripotiwa kutumia gari la serikali kuwasafirisha watu waliokosa magari baada ya Matatu kugoma, huku wakilipisha bei ghali, wateja ambao hawakuwa na namna.

Polisi hao, ambao wengine walikuwa na sare rasmi za kazi wanadaiwa kubeba wateja kutoka mji wa Marigat, na kuwalipisha hadi Sh400, mahali ambapo kwa kawaida huwa Sh200.

Hali hiyo ilisemekana kuchochea malalamishi miongoni mwa wahudumu wa Matatu ambao walikuwa kazini baada ya kuona ushindani kutoka kwa maafisa wa serikali ambao hawajaruhusiwa kufanya biashara hiyo.

Gari lenyewe lilikuwa aina ya Land Cruiser GKB 689. Baadhi ya wateja walisema kuwa polisi hao ambao walikuwa wakielekea mjini Nakuru kazini waliwaambia kuwa wangetaka kuwasaidia wale waliokuwa na Sh400 kulipia huduma ya usafiri.

Gari hilo linasemekana kuwabeba wateja Zaidi ya 10, wakiwemo watoto. Watu katika barabara hiyo hawakuwa na namna baada ya Matatu kugomea kazi.

“Hatukuwa na tatizo kupanda gari hilo kwa kuwa tulikuwa tumekaa barabarani sana,” akasema mama mmoja ambaye hakutaka kutambulishwa.

Gari hilo linasemekana kwenda likiwashusha wateja hao kutoka eneo la London, kwenye viunga vya mji wa Nakuru hadi kati ya mji.

Lakini Mkuu wa trafiki kanda ya Bonde la Ufa alisema maafisa hao walikosea kwani gari la polisi halipaswi kutumiwa kwa kazi za kubeba kama Matatu.