Wahudumu wa teksi wakosa adabu kwenye viwanja vya ndege kuadhibiwa
NA CHARLES WASONGA
WAHUDUMU wa teksi ambao watapatikana na hatia ya kuwasumbua wateja katika viwanja vya ndege humu nchini wataadhibiwa kupitia kufutiliwa mbali kwa leseni zao za kuhudumu katika maeneo hayo, Waziri wa Uchukuzi James Macharia alitangaza Jumanne.
Vile vile, waziri huyo alisema wahudumu hao watakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na Halmshauri ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA).
Bw Macharia alisema hayo Jumanne alipokuwa alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi Mwanamke wa Lamu Bi Ruweida Mohamed Obbo (pichani kati).
Mbunge huyo alikuwa amelalamikia tabia ya wahudumu wa teksi ya kung’ang’ania abiria katika viwanja vya ndege vya Jomo Kenyatta (JKIA) na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi, Mombasa.
“Binafsi nimekuwa nikisumubuliwa kila mara na wahudumu hawa wa teksi kila mmoja akitaka niabiri gari. Huwa wamesimama nje ya eneo ambako abiria huondokea baada ya kushuka kwa ndege. Watu hawa ni hatari kwa usalama wa abiria, katika JKAI na Moi ambazo ni sura ya taifa hili,” akasema Bi Obbo.
Naye Bw Macharia akajibu, “Shughuli ya utoaji wa leseni kwa wahudumu wa teksi hutolewa na mamlaka ya KAA. Nimeishuri kufutilia mbali leseni za wahudumu ambao wataendelea kuwasumbua abiria katika viwanja vya ndege kote nchini na haswa uwanja wa JKIA.”
Waziri alisema wizara yake kupitia mamlaka ya KAA itahakikisha kuwa hali ni shwari katika uwanja wa JKIA haswa wakati huu ambapo imepandishwa hadhi ya kuweza kupokea ndege moja kwa moja kutoka Amerika.