Kimataifa

Shinikizo zaisukuma Uchina kuendeleza marufuku ya pembe za vifaru

November 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

UCHINA imetangaza kuwa itasongesha muda wa kuondoa marufuku ya kuingizwa kwa pembe za vifaru, baada ya uamuzi wake kuvutia kilio na kukashifiwa kutoka kote duniani, haswa kutoka kwa mashirika ya kimazingira.

Mashirika hayo yalilalamika kuwa Simba marara na Vifaru ni wanyama ambao wako kwenye hatari ya kuisha, na hivyo kuruhusu pembe na ngozi zao kuuzwa nchini humo ni sawa na kuunga mkono uwindaji wao haramu.

Mwezi uliopita, China ilitangaza kuwa itaruhusu sehemu za wanyama hao kutumiwa kwa tafiti za kisayansi na shughuli za kitamaduni. Ilikuwa imesema kuwa sehemu hizo zingetumiwa kwa ajili ya matibabu vilevile.

Hata hivyo, sasa nchi hiyo imetangaza kuwa imesongesha mbele hatua hiyo “baada ya utafiti.”

Kupitia habari iliyotolewa na afisa mkuu wa serikali Jenerali Ding Xuedong, China ilisema marufuku ya bidhaa hizo itaendelea japo haikutaja kwa kipindi kipi.

“Serikali ya China kwa muda mrefu imekuwa ikipigania ulinzi wa wanyama pori na imepiga hatua ambazo dunia inatambua,” akasema Bw Ding.

Baada ya habari hizo, shirika la kimataifa la kupigania ulinzi wa wanyama pori WWF lilisema hatua hiyo ya China ni “ishara njema kwa kilio cha kimataifa.”

“Kuruhusu biashara ya hadi wanyama walio kwenye hatari ya kuisha kungekuwa na matokeo mabaya kwa idadi ya Vifaru na Simba Marara,” shirika la WWF likasema kupitia ujumbe.