• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Baada ya Canada kuhalalisha bangi, sasa zao hilo halipatikani

Baada ya Canada kuhalalisha bangi, sasa zao hilo halipatikani

MASHIRIKA na PETER MBURU

MONTREAL, CANADA

TAYARI nchi ya Canada imeanza kushuhudia upungufu mkubwa wa zao la bangi, wiki tatu tu baada ya kuhalalisha matumizi ya bidhaa hiyo kwa njia za kimatibabu.

Kufuatia hivyo, baadhi ya wateja ambao wamegadhabishwa na hali hiyo sasa wamelazimika kutafuta bidhaa hiyo katika masoko haramu ili kujiburudisha.

Angalau mikoa mitatu- Ontario, Quebec na New Brunswick- inashuhudia upungufu mkubwa wa bangi halali, huku baadhi ya maduka yaliyokuwa yakiuza yakifungwa kwa kukosa bidhaa hiyo.

Wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wamesema kuwa wakulima hawakukuza zao la kutosha, wala hawana vifaa vya kutosha vya kupakia zao hilo ili kulifikisha sokoni.

Upungufu huo sasa umeonekana kama utakaotishia lengo la awali la kuhalalisha soko hilo, ambalo lilikuwa kumaliza soko haramu, ambalo limekuwa likishiriki katika biashara ya dola 5.3bilioni za Canada kila mwaka.

Lakini watumizi wenye ghadhabu wamesema kuwa sasa wamelazimika kurejea kwa wauzaji haramu ambao walikuwa wakiwauzia mbeleni, huku wauzaji wengi haramu wakitumia fursa hiyo ya upungufu kuchuuza bangi manyumbani tena kwa bei rahisi.

Watumizi na wauzaji wote wamedokeza kuwa upungufu huo umeshuhudiwa kufuatia hatua ya seikali kuhalalisha uuzaji wa bangi, jambo ambalo lilisababisha maelfu ya watu kumiminika sokoni kununua bidhaa hiyo, kinyume na ilivyotarajiwa.

“Tunajenga soko jipya ambalo halikuwepo wiki tatu zilizopita na tulijua kutakuwa na changamoto,” akasema Mathieu Gaudreault, msemaji wa shirika la bangi, Quebec.

Alisema kuwa kiwango cha uhitaji wa bangi kilizidi kile cha usambazaji, na kuwa wazalishaji walio na leseni walipeana makadirio makubwa kuliko uwezo wao.

Kutokana na hilo, alisema kuwa sasa wazalishaji wanaweza kuongeza idadi ya watu wa kuzalisha zao hilo ili kukabili kiwango kikubwa cha uhitaji sokoni.

Shirika hilo la bangi Quebec lilifikia uamuzi wa kufunga matawi yake 12 ya kuuza bangi siku tatu kwa wiki, hadi kiwango cha usambazaji kirejelee hali ya kawaida.

Hali imezidi kuharibika katika mikoa mingine kama New Brunswick ambao ulifuata mkondo wa Quebec, baada ya upungufu kuingia huko pia.

Mkoa wa Ontario aidha umeshuhudia hali ya wanunuzi kurejea kwa wauzaji haramu kufuatia upungufu huo. Katika wiki ya kwanza ya kuhalalishwa kwa bangi, duka la serikali mkoa huo lilipokea manunuzi 150, 000 ya oda na limekuwa likipambana kutafuta bidhaa za kukidhi manunuzi hayo hadi leo.

“Serikali inazidi kutoa nafasi kwa wateja kwenda katika soko haramu kwani upungufu umesababisha hivyo. Bangi halali inaletwa kwa uchache mno kiwango kuwa hakuna anayeburudika nayo,” akasema Bw Tobin, muuzaji wa duka moja la bangi.

Alisema kuwa bidhaa zake zote zilinunuliwa kwa muda wa saa nne punde tu alipofungua duka lake, siku bangi ilihalalishwa mnamo Oktoba 17.

Hata hivyo, alisema kuwa amekuwa akilazimika kufunga duka lake kwa muda mrefu kutokana na hali ya kukosa bidhaa kwani wasambazaji hawako.

Wasemaji wa serikali wamekiri kuwa hata wakati iliporuhusu biashara hiyo baada ya kuiharamisha kwa miaka mingi, serikali haikufanya utafiti wa kutosha kujua ni bidhaa zipi zilizohitajika sana sokoni na kwa kiwango kipi.

You can share this post!

ERC yaongeza bei ya mafuta tena

Uongo aliotumia mama wa miaka 62 kupata mimba

adminleo