• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
NASA ILIVYONASWA

NASA ILIVYONASWA

BENSON MATHEKA Na MWANGI MUIRURI

SERIKALI ya Jubilee ilitumia mbinu ya kugawanya na kutoa ahadi katika juhudi zake za kunasa waliokuwa viongozi wa Muungano wa NASA kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Mikakati hiyo ilibuniwa wakati muungano huo ulipokuwa umeonekana kuchukua msimamo mkali baada ya uchaguzi wa 2017, na ikaonekana mbinu pekee ilikuwa ni kuvunja mshikamano wa aliyekuwa mgombeaji urais wa NASA Raila Odinga, mgombeaji mwenza Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula.

Wakati wakuu hao walipotangaza kuwa wangemwapisha Bw Odinga kuwa “rais wa wananchi”, wapangaji mikakati wa Jubilee walitumia kila mbinu kuhakikisha mgawanyiko umeibuka.

“Tulianza kwa kuwanyemelea Mudavadi, Kalonzo na Wetang’ula ambapo tuliwashawishi wasusie kiapo cha Raila,” Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu aliambia Taifa Leo. “Baada ya kujiapisha tulihakikisha kuwa Raila amepata fununu kuwa tulikuwa na nia ya kuwaita wandani wake watatu wakutane na Rais Uhuru Kenyatta. Hapo Raila alibabaika akihofia kuwa angetengwa. Alikuwa hana lingine ila tu kufanya hima awe wa kwanza kukutana na Rais. Hapo ndipo njama yetu ilifanikiwa,” akasema.

Baada ya Rais Kenyatta kufanikiwa kumweka makwapani Bw Odinga, Serikali ilifanikiwa kuchapa upinzani kiboko kwa kuwaacha vinara watatu waliobakia wakitapata.

Hatua ya pili ilikuwa ni kukosanisha vyama tanzu vya NASA kwenye bunge ambapo hatua hiyo ilifanikiwa kwa kuchochea kutimuliwa kwa Bw Wetang’ula kutoka cheo cha kinara wa wachache kwenye Seneti.

Mbinu ambazo zilitumiwa kumuondoa Bw Wetang’ula zilikuwa za kumuaibisha, hatua ambayo ilileta uadui wa kisiasa kati yake na Bw Odinga. Kwa sasa Seneta huyo wa Bungoma anaonekana kuwa na uhusiano wa karibu na Naibu Rais William Ruto.

Baada ya kuona Bw Odinga amevuka peke yake na kushikana na Jubilee, Bw Musyoka naye aliyeyuka roho na kutangaza kuunga mkono serikali. Kilele cha haya kilikuwa ni kuingizwa “boksi” alipotangaza atakuwa “mtu wa mkono wa Rais”. Kati ya vinara hao wa NASA, ni Bw Mudavadi pekee ambaye hadi sasa amesimama kidete, lakini uwezo wake wa kukataa kunaswa utajulikana muda unavyosonga.

Ahadi za vyeo vya juu pia zilichangia wakuu wa NASA kunaswa na sasa wanafurahia matunda ya kuingia kambi ya Jubilee. Bw Odinga sasa ni Mjumbe Maalum wa Muungano wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi huku Bw Musyoka akitarajiwa kuwa mpatanishi mkuu Sudan Kusini.

 

MAISHA YA KIFAHARI

Ahadi ya maisha ya kifahari pia imejitokeza kuwa chambo iliyonasa wawili hao. Kwa sasa wanafurahia ulinzi kutoka kwa serikali, magari ya kuandamana nao wanaposafiri miongoni mwa matunda mengine ya kuimba wimbo wa serikali.

Wadadisi wanasema Bw Odinga na Bw Musyoka huenda pia walinaswa baada ya kugundua kwamba itawachukua miaka 10 kuwa katika baridi ya kisiasa, hali ambayo hawajazoea, na ndipo wakaamua kuchangamkia serikali.

Katika kutetea uamuzi wake, Bw Odinga amekuwa akisema aliamua kuunga mkono Serikali katika juhudi za kumaliza siasa za migawanyiko ambazo zimekuwepo nchini kwa muda mrefu.

Lakini licha ya kuleta utulivu wa kisiasa, kufaulu kwa Rais Kenyatta kunasa NASA kumezua hofu kuwa Kenya inarejea katika utawala wa chama kimoja kwa kukosa upinzani wenye makali ya kukosoa serikali.

Baadhi ya wafuasi wa NASA pia wanahisi kuwa wawili hao waliwasaliti kwa kuweka mbele maslahi yao ya kibinafsi.

Ingawa haijajitokeza kama pia amenaswa, Naibu Kiongozi wa ODM Gavana Hassan Joho wa Mombasa naye amekomesha lawama zake dhidi ya Jubilee.

Wiki jana, Bw Joho aliandamana na Rais Kenyatta hadi mjini Paris, Ufaransa kuhudhuria kongamano la kimataifa kuhusu hali ya hewa ulimwenguni.

Wabunge wa NASA nao, ambao walikuwa wakosoaji wa serikali, nao wamekuwa wakiunga mkono ajenda za serikali bungeni.

You can share this post!

KASHFA YA NYS: Malumbano mahakamani

Yafichuka Barcelona ilikataa huduma za Kylian Mbappe

adminleo