• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Sherehe za harusi zanogesha biashara

Sherehe za harusi zanogesha biashara

Na WINNIE ATIENO

BIASHARA katika hoteli nyingi nchini zinaendelea kunoga kutokana na sherehe za harusi, zile za kufunga mwaka na za kuzaliwa kwa watoto.

Baadhi ya wakuu wa hoteli walisema wanaendelea kupokea wageni kutokana na sherehe hizo pamoja na kampuni zinazowaandalia wafanyikazi wao sherehe za kufunga mwaka

Mkurugenzi mkuu wa hoteli ya PrideInn Westlands, Andrew Makau aliiambia Taifa Leo kuwa, maharusi wanafunga mwaka kwa kufanya harusi za kata na shoka katika hoteli za kifahari jijini Nairobi huku sekta hiyo ikiendelea kuimarika.

Bw Makau alisema licha ya kuwa sekta ya utalii hunoga eneo la Pwani wakati wa likizo ya Disemba, hoteli jijini Nairobi zinaendelea kuwa na shughuli nyingi kutokana na biashara ya kuandaa sherehe, hususan za harusi.

“Hoteli za jijini Nairobi zinaendelea kupokea biashara nyingi licha ya watalii wa humu nchini na wageni kufurika kaunti ya utalii ya Mombasa. Huu ni wakati wa wachumba kufanya harusi hadi Disemba kabla sherehe za Krisimasi,” alisema mkurugenzi huyo mkuu wa hoteli hiyo iliyoko jijini Nairobi.

Bw Makau alisema hoteli zinaendelea kupokea biashara nyingi kutoka kwa wanawake wajawazito wanaofanya sherehe za watoto maarufu kama ‘baby showers’ na sherehe za kabla harusi.

Alisema mamia ya wapenzi wanaendelea kushika nafasi za hoteli tayari kwa sherehe za harusi.

“Watu wengi wanapenda mwezi wa Disemba ili kufunga harusi sababu ni mwezi wa likizo ambapo familia nyingi hukongamana sehemu moja,” akaongeza.

Alisema sherehe hizo zimefanya hoteli nyingi kuwa na biashara.

“Licha ya kuwa watu hupenda kwenda Mombasa kwa likizo ya Disemba ikilinganishwa na Nairobi, mwaka huu harusi na sherehe hizo zimefaidi hoteli zetu ,” alisema mhudumu huyo katika sekta ya utalii.

Alitaja wapiga picha, wapishi, wapambe, waandalizi wa sherehe, wauzaji maua, bendi za muziki, wamiliki wa sehemu za sherehe, kampuni za kukodisha magari ya kifahari kuwa miongoni mwa sekta ambazo zinaendelea kupokea biashara nyingi.

“Wale wote walio na kampuni za kushughulikia mipango ya harusi zinazowapendeza maharusi wanafaa wahakikishe wanavuna wakati huu ambapo biashara imenoga kabla ya mwezi wa ukame wa Januari, ambapo mapato ya kibiashara hukauka,” alisema Bw Jackton Amutala, meneja wa hoteli za PrideInn jijini Nairobi.

Bw Amutala alisema idadi ya harusi zinazoandaliwa katika hoteli za kifahari zinaongezeka kila kuchao.

“Tunafurahia biashara nyingi tangu Oktoba, hoteli yetu imekuwa ikiandaa angalau harusi mbili kila wikendi. Ifikapo Disemba, tutakuwa na harusi nne kila wikendi hususan siku ya Jumamosi. Zingine tunakodishwa kutoa huduma za vyakula na vinywaji,” Bw Amutala alisema.

Katika siku za hivi karibuni, wapenzi wamekuwa wakiandaa harusi zao katika hoteli za kifarahi ili kufurahisha jamaa na marafiki zao huku mitandao ya kijamii kama Instagram, Twitter na Facebook, ikisaidia sekta ya hoteli kupokea biashara.

Huko Pwani sekta ya utalii nayo imenoga hususan wakati wa likizo huku wanafunzi wengi wakielekea Mombasa kuogelea kwenye fuo za Bahari Hindi.

You can share this post!

Kibaki asheherekea miaka 87 kimya kimya nyumbani kwake

KINAYA: Raia wa kawaida ni kama wakimbizi nchini mwao,...

adminleo