• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
KINAYA: Raia wa kawaida ni kama wakimbizi nchini mwao, wanasiasa hawawajali!

KINAYA: Raia wa kawaida ni kama wakimbizi nchini mwao, wanasiasa hawawajali!

NA DOUGLAS MUTUA

MWANA wa Jomo hana matiti ya kumnyonyesha mtu! Ana nini? Chupa nne za maziwa, yaani kama anayonyosheshwa mtoto mchanga akilia sana.

Lo! Tayari mbili zimetwaliwa! Na nani? ‘Baba’, yule mzee aliyekataa kurejea mashambani Bondo, ana moja.

Na ya pili ina nani? Mwite Wiper ataitika, sikwambii anainyonya sawasawa kwa maana yake ni mpya.

Ya tatu na ya nne? Zinawasubiri MaDVD na Weta, wakisusa warejee magharibi mwa nchi walikotoka wakatafute ilikoivia ‘busaa’, wapige mafunda kadha ili wayasahau masaibu yanayowasibu!

Ikiwa ulidhani mojawapo ya chupa hizo ingepewa makabwela wa Jubilee, basi unahitaji ukaguzi fulani kuanzia shingo kwenda juu.

Siku hizi hakuna Jubilee wala NASA, sote ni Wakenya. Hata labda tayari karatasi za kura tulizopiga zishageuzwa shashi na kutumika vyooni! Ala! Kweli? Naam, uhusiano kati yako na watu uliochagua uliishia kwenye debe.

Hata nyimbo na kaulimbiu za kipuuzi kama “Tano Tena!” na Tibiim! Tialala” siku hizi, kwenye masikio ya wanasiasa, ni uchafuzi wa mazingira unaopaswa kuchunguzwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA).

Hayo amesema nani? Mwanasiasa kwa vitendo, si mimi. Na ukumbuke vitendo hunena kwa sauti kuu kuliko maneno yanayotoka kinywani.

Mkenya popote alipo, ikiwa si mbunge au mwanasiasa anayezoa mamilioni ya pesa, si chochote nchini mwake! Hata afadhali mkimbizi anayetetewa na mashirika ya kimataifa.

Hivi chupa za maziwa anazotoa mwana wa Jomo zinakusudiwa nini? Kuwanyamazisha kina domo-kaya waliobweka na kuvuruga karamu ya kuitafuna Kenya.

Kumbuka Kenya inaliwa na Wachina wakisaidiwa na ‘walinzi wa nyumbani’ wa kisasa, sawa na ilivyofanyika wakati wa ukoloni. Mchina hataki kelele akiimega keki Kenya.

Nafasi ya Mkenya wa kawaida iko wapi hasa kwenye meza kubwa ya kuimega nchi yake? Nimekwambia, na nitarudia, kwamba Mkenya wa kawaida ni kama mkimbizi!

Wanaofaidi maziwa ya chupa ni wawakilishi wa wakimbizi. Wamekwenda kuwatafutia mamilioni ya maskini hao angaa punje kadha za mahindi ya njano.

Halafu? Wakaambiwa tulieni, mnahitaji kutia kitu tumboni ili mpate nguvu za kurejea mlikotoka.

Kisha? Mwisho wa kunyonya wataambiwa wamenyonya hata mahindi ya wakimbizi, waondoke kimyakimya au dunia itangaziwe yanavyonuka mashuzi yao wakinywa maziwa!

Na hawatakuwa na lao ila kuondoka kimya kwani waliacha wajibu wao wa mwanzo, wakashibisha matumbo yao kwanza.

Mwana wa Jomo amejua ghala la kitaifa halina kitu, hata sarafu chache za nchi tunazoficha chini ya godoro zimekwisha, akaamua kutupumbaza.

Sasa Kenya haina upinzani, hivyo akiamua kutuhasi au kurejesha sheria za Kanu ya Mzee Kirungu hakuna wa kututetea. Watu wangali wananyonya maziwa, kumbuka!

Asiye na wake ana nani? Bila shaka ana Mungu, ambaye atatupa njia ya kujikomboa kutoka utumwa wa kuwategemea wazee walafi watutetee.

Nitasema wazee wanyonye chupa kabisa, shida zituume kwelikweli kama chawa au kunguni wa jela, tupate akili zetu na kukurupuka mara moja ili tujikomboe!

Binadamu huzaliwa huru, lakini uzembe wake humfanya kumkabidhi binadamu mwenzake jukumu la kumkomboa. Shika adabu yako!

[email protected]

You can share this post!

Sherehe za harusi zanogesha biashara

TAHARIRI: Masoko zaidi ya mazao yasakwe

adminleo