Naibu Gavana hatarini kupoteza wadhifa
Na BERNARDINE MUTANU
Wawakilishi wa wadi katika Kaunti ya Machakos walipiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya afisa mkuu wa fedha Francis Maliti.
Bw Maliti pia ndiye naibu gavana wa Kaunti ya Machakos. Hii ni baada ya Bunge la Machakos kuidhinisha ripoti ya kamati ya muda iliyohusu kuondolewa kwa Bw Maliti kama afisa mkuu msimamzi wa fedha katika kaunti hiyo.
Bw Maliti aliondolewa na wawakilishi 35 ilhali wengine 24 walikataa kufika kwa kikao hicho.
Akihutubia wanahabari nje ya afisi yake Jumatatu, Gavana Alfred Mutua alisema hatua hiyo ilikuwa ya kisiasa.
Licha ya kuondolewa na wawakilishi, Gavana Mutua alisema Bw Maliti angeendelea kuwa afisa mkuu wa fedha katika kaunti hiyo.
Kulingana na gavana huyo, wawakilishi hao walitekeleza hatua hiyo ili ‘kuendeleza ufisadi’.