Polisi wang'oa bangi ya Sh15 milioni Migori
Na PETER MBURU
POLISI katika kaunti ya Migori Alhamisi waling’oa bangi ya thamani ya Sh15 milioni katika shamba moja.
Baada ya kupata habari kutoka kwa umma, maafisa hao walivamia shamba hilo la ukubwa wa ekari moja kijiji cha Riangora, eneo la Suna Magharibi, karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania na kung’oa mimea hiyo yote.
Wamiliki wa shamba hilo wanasemekana kuwa wasambazaji wakuu wa bangi eneo la Nyanza.
Kaunti ya Migori imekuwa ikitumiwa kama njia ya wafanyabiashara wa dawa hiyo ya kulevya kupitisha bangi kue;lekea Jijini Nairobi na miji mingine mikubwa ya humu nchini.
Nyingi za bangi hutoka taifa jirani la Tanzania na kutoka kwa wakulima wa Kenya ambao wanaikuza maeneo ya mpakani.
Maafisa hao aidha walinasa magunia ishirini ya bangi ambayo tayari ilikuwa imevunwa na ilikuwa tayari kusafirishwa.
Kamanda wa polisi Migori Julius Amariko alisema kuwa maafisa wake walipata habari kutoka kwa watu wa nia njema na kukimbia katika kijiji hicho alfajiri.
Baadhi ya wafanyakazi ambao walikuwa shambani walitoroka walipowaona polisi.
“Bangi hiyo ilikuwa imepandwa ndani ya shamba la mahindi na washukiwa ambao wanasemekana kuwa watu wa familia moja walitorokea taifa jirani la Tanzania. Ile iliyokuwa imevunwa tayari ilikuwa imefichwa nyumbani,” akasema Bw Amariko.
Wakazi wa eneo hilo sasa wameshauriwa kuwacha kuuza bangi.
“Kile kimetokea leo kinashangaza na tumekuwa tukiwaambia watu waaache kuuza bangi,” akasema naibu kamishna wa Suna Magharibi Mballa Mutua.