• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Vidhibiti mwendo sasa vyaisha madukani

Vidhibiti mwendo sasa vyaisha madukani

Na BONIFACE OTIENO

UKOSEFU wa vidhibiti mwendo katika magari ya usafiri wa umma umesababisha asilimia 40 ya matatu kuendelea kulala kwenye gereji baada ya hatua ya polisi kuanzisha msako dhidi ya magari mabovu barabarani tangu Jumatatu iliyopita.

Muungano wa Wamiliki wa Matatu (MOA) umesema kuwa wengi wa wahudumu wao bado hawajarejelea kazi tangu operesheni hiyo ilipoanzishwa, huku kukiwa na upungufu wa vifaa hivyo sokoni, licha ya watu wengi kuvihitaji kwa sasa.

“Hakuna ajenti anayeuza Vidhibiti mwendo katika soko la Kenya kwa sasa. Manne ya magari yangu yamelala nyumbani kwa sasa kutokana na hali hiyo,” akasema mwenyekiti wa MOA Simon Kimutai.

Aliongeza kuwa bei ya vifaa hivyo imeongezeka kutoka Sh10,000 hadi Sh15,000 na kusema kuwa vifaa hivyo viliisha sokoni Ijumaa wiki iliyopita.

Bw Kimutai alielezea wasiwasi wa wahudumu kuwa vifaa vingine vinatarajiwa baada ya wiki tatu.

Jumatatu na Jumanne wahudumu wa matatu waliondoa magari yao barabarani ili kuepuka operesheni iliyokuwa ikiendelezwa na hadi sasa idadi kubwa ya magari hayo bado haijarejea barabarani.

Hali hiyo imechangia nauli katika mabasi kupanda kwa viwango vikubwa, huku wahudumu wa teksi na Uber nao wakivuna kutokana na uchache wa magari ambao unashuhudiwa hadi sasa.

Kwa upande wao, mekanika nao wanasema kuwa vidhibiti mwendo vimeisha baada ya wahudumu wa magari ya usafiri wa umma kuvinunua kwa wingi sana katika harakati za kuzingatia sheria za Michuki ambazo zimerejeshwa barabarani kama mbinu ya kurejesha urazini katika sekta ya uchukuzi.

“Hakuna vidhibiti mwendo sokoni na itachukua takriban wiki mbili kupata vingine,” akasema Bw George Obiero ambaye ni mekanika jijini Nairobi.

Mwezi uliopita, mawaziri wa uchukuzi James Macharia na wa Usalalama wa Ndani Fred Matiangi walitangaza kurejea kwa sheria za Michuki na kuwapa wahudumu wa magari ya usafiri wa umma hadi Novemba 12 kuzizingatia kikamilifu.

You can share this post!

Nusu ya watahiniwa wa ualimu wafeli vyuoni

Wanaume 4 kizimbani kwa kumteka nyara polisi wa kike

adminleo