Aliyedandia meli 1991 Kilindini na kupotea atafutwa
Na SAMUEL BAYA
Familia moja katika eneo la Mtongwe, Mombasa sasa inatafuta usaidizi wa kumpata mwanao aliyepotea mwaka wa 1991.
Inaaminika kuwa kijana huyo alidandia meli moja ya mizigo iliyokuwa ikiondoka katika bandari ya Kilindini, Mombasa.
Sasa familia ya Shaban Khamisi ambaye akiondoka nyumbani alikuwa na umri wa miaka 18 inaitaka serikali iwasaidie kumtafuta aliko kwani kuna wakati ilipata habari kuwa yuko nchini Ujerumani.
Akiongea na waandishi wa habari katika kijiji cha Mweza, Mtongwe, katika eneo la Likoni, jana mamake Shabaan Bi Asha Suleiman alisema kuwa tangu mwanawe apotee miaka 27 iliyopita, maisha yake yamekuwa magumu kupindukia.
“Mimi ninaishi kwa majonzi. Sijui mwanangu yuko wapi. Nimelia na hata sasa sijawahi kupata jibu. Ni nani ambaye atanisaidia kumpata mwanangu,” akasema ajuza huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80.
Huku akionekana mwingi wa mawazo, bi kizee huyo alisema kuwa baadhi ya wanajamaa ambao kijana wake aliwaacha sasa wamefariki na hajui hata kama mwanawe yuko hai huko aliko.
“Mimi ninachokumbuka ni kuwa mwanangu alikuwa akifanya vibarua katika bandari ya Mombasa na aliondoka asubuhi hiyo asirudi tena.
Nilikuwa na matumaini lakini hadi leo hii sijajua kama huko aliko yuko hai au alifariki. Nimezoea sasa kumkosa lakini kama mama, niko na uchungu mwingi sana,” akasema Bi Suleiman.
Shemeji ya Shaban Mzee Abdalla Sharbaid aliambia Taifa Leo kwamba kijana huyo alikuwa akifanya kazi kama kibarua katika bandari ya Mombasa.