• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Raila aanza kazi rasmi AU, ahudhuria kikao Ethiopia

Raila aanza kazi rasmi AU, ahudhuria kikao Ethiopia

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga, ameanza rasmi kuchapa kazi yake mpya katika muungano wa AU, ambayo alipata wiki mbili zilizopita.

Bw Odinga Jumamosi alihudhuria kongamano spesheli la muungano huo jijini Addis Ababa, Ethiopia ambalo linanuia kuanza kuweka mikakati ya kufufua AU kuipa nguvu tena kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Alihudhuria siku chache tu baada yake kuteuliwa kuwa Mjumbe Maalum wa kusimamia Ujenzi wa barabara na miundomsingi barani Afrika, wadhifa ambao umeundwa kwa mara ya kwanza.

Bw Odinga jana alichapisha picha tatu katika akaunti yake ya Twitter, moja akiwa katika jumba la kongamano hilo akifuatilia mazungumzo, nyingine wakiwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na nyingine ya Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia kongamano.

Vilevile, Bw Odinga alikuwa pamoja na bintiye Winnie Odinga katika kongamano hilo, ambaye katika picha moja alikuwa ameketi nyuma yake ndani ya jumba la kongamano.

“Ninahudhuria kongamano maalum la 11 la AU ambalo linaangazia mageuzi na kuuunda vizuri muungano wa bara. Aidha Marais Cyril Ramaphosa na Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa wengine wanahudhuria,” Bw Odinga akaandika Twitter.

Haijulikani ikiwa Bw Odinga na Rais Kenyatta walisafiri pamoja kuelekea Ethiopia, lakini kongamano hilo ambalo linakamilika leo, lilikuwa la Marais ama mawaziri teule kuwakilisha nchi zao.

Kazi yake mpya imekuja na hadhi ya juu kwani Bw Odinga atakuwa na ofisi tano barani, katika mataifa ya Afrika Kusini, Nigeria, Ethiopia, Kenya na Misri.

Japo ni kazi iliyokuja na majukumu mengi, Bw Odinga tayari amesema kuwa haitamwathiri kujihusisha na siasa za humu nchini.

Rais Kagame ndiye kiongozi wa msukumo huo wa kuupa nguvu tena muungano wa AU na kuukomboa kutokana na kuingiliwa na mataifa ya magharibi.

Kuanza kwa Bw Odinga kazi hiyo kumekuja wakati kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka naye akiteuliwa kuongoza juhudi za kutafuta amani Sudan Kusini, baada ushirikiano wao na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Musyoka bado anasubiri kuapishwa na muungano wa IGAD ili kuanza kazi yake rasmi, lakini tayari amekutana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.

You can share this post!

Polisi watumbua jipu la ulanguzi wa binadamu Nairobi,...

UAVYAJI MIMBA: Marie Stopes yazimwa

adminleo