• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
2022: Kindiki amshauri Muthomi akome kufikiri ugavana ni wa mtu mmoja

2022: Kindiki amshauri Muthomi akome kufikiri ugavana ni wa mtu mmoja

Na ALEX NJERU

SENETA wa Tharaka-Nithi, Kithure Kindiki amemwambia Gavana Muthomi Njuki kukoma kulalamika kuhusu njama za kumwondoa mamlakani ifikapo 2022 kwani hakuna nafasi ya uongozi ambayo ni ya mtu binafsi.

Akizungumza Jumapili katika kijiji cha Kathangacini, eneobunge la Tharaka, Prof Kindiki alisema kila mtu yu huru kuwania nafasi yoyote ila sharti awape walio uongozini nafasi ya kuwahudumia wananchi.

“Hakupaswi kuwa na hali ya chuki wakati mtu fulani anapotangaza nia ya kuwania wadhifa wowote. Hata hivyo, lazima walio mamlakani wapewe nafasi ya kuutumikia umma,” akasema.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubu katika mazishi ya Stella Gatiiria, mamaye diwani wa wadi ya Gatunga, Muutegi Ruujia.

Gavana Njuki amekuwa akilalamika kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa wakiendesha kampeni za mapema dhidi yake.

“Huu ni wakati wa kuwahudumia wananchi. Tunapaswa kungoja kampeni hadi 2022,” akasema.

Seneta huyo, ambaye alifika muda mfupi baada ya Bw Njuki kuhutubu, alisema kuwa kungali na viongozi wengi ambao watachaguliwa na wananchi kuwahudumia ifikapo 2022.

Kindiki aliwaomba viongozi wa kaunti hiyo kuungana, akisema kuwa yuko tayari kushirikiana na viongozi wote kwa lengo la kuimarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

“Kwa ustawi wa eneo hili, lazima tuepuke malumbano ya mara kwa mara ambayo yanakwamisha ustawi wa eneo hili,” akasema.

Alieleza kuwa lazima viongozi wote waungane na kushauriana, kwani hakuna anayefahamu kila kitu.

Wawili hao wanaonekana kuwa wagombea wakuu wa ugavana, ijapokuwa Prof Kindiki hajatangaza wazi ikiwa atawania nafasi hiyo.

You can share this post!

Waumini 100 waabudu kando ya barabara

Lazima niwe debeni 2022 – Moi

adminleo