• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Lazima niwe debeni 2022 – Moi

Lazima niwe debeni 2022 – Moi

Na FRANCIS MUREITHI

SENETA Gideon Moi wa Baringo amesema kwamba ndiye atakayekuwa mgombea urais wa chama cha KANU mnamo 2022.

Akihutubu kwenye harusi ya mbunge wa Samburu Magharibi, Naisula Lesuuda mnamo Jumamosi, Bw Moi alisema kuwa hakuna sababu yoyote ambayo itazuia chama hicho kutwaa uongozi kwenye uchaguzi huo.

Bw Moi alisema chama hicho kimejitayarisha vilivyo kukabiliana na washindani wake, hivyo hakitatishika kwa vyoyote vile.

“Nawaomba wakazi wa Samburu kuendelea kuonyesha imani yao kwa Kanu. Nawaomba kunipigia kura ifikapo 2022, kwani mimi ndiye nitakayekuwa mwaniaji wake wa urais,” akasema.

Kiongozi huyo alisema kuwa yuko tayari kukiimarisha chama chake kabla ya uchaguzi huo, ili kuhakikisha kimepata umaarufu kamili wa kisiasa.

Bw Moi amekuwa akiangaziwa pakubwa, kwani viongozi mbalimbali wa kisiasa wamekuwa wakimtembelea Rais Mstaafu Daniel Moi nyumbani kwake Kabarak.

Miongoni mwa viongozi ambao wamemtembelea Mzee Moi, aliye babake Gideon ni kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka kati ya wengine wengi.

Wadadisi wa kisiasa wamekuwa wakizitaja ziara hizo kama matayarisho ya kumwandaa Bw Moi kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapong’atuka uongozini.

Lakini akizungumza katika hafla hiyo, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alimwambia Bw Moi kujitayarisha kwa ushindani mkali kutoka kwa Naibu Rais William Ruto ambaye pia ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.

“Kinyang’anyiro cha 2022 hakitakuwa ushindani wa kisiasa wa kawaida. Bw Moi atakumbwa na kibarua kigumu kumkabili Bw Ruto,” akasema Bw Kuria.

Hata hivyo, mbunge wa Tiaty, William Kamket, aliye mshirika wa karibu wa Bw Moi alisema kuwa seneta huyo ndiye anayefaa zaidi kumrithi Rais Kenyatta.

“Bw Moi ndiye atakayekuwa mgombea urais wa Kanu. Nawaomba Wasamburu na jamii zote za kuhamahama kumpigia kura Bw Moi kwani hana sakata yoyote ya ufisadi inayomwandama,” akasema Bw Kamket.

Wabunge 18 kutoka chama cha Jubilee (JP) na upinzani, magavana watatu kati ya viongozi wengine walihudhuria hafla hiyo ya kufana.

Bi Lesuuda aliolewa na mpenziwe wa muda mrefu, Bw Robert Koitaba.

Hafla hiyo ilifanyika nyumbani kwa mbunge huyo katika eneo la Lesirai, Seguta Marmar, Kaunti ya Samburu.

You can share this post!

2022: Kindiki amshauri Muthomi akome kufikiri ugavana ni wa...

Thamani ya shilingi ya Kenya yaporomoka

adminleo