Wakataa vinyozi vya Muchomba wakisema ni vya thamani ya chini
Na Mary Wambui
WANACHAMA wa Muungano wa Vinyozi wa Thika wamekataa kupokea vifaa vyenye thamani ya Sh1 milioni vilivyotolewa kwao kwa mkopo na Mbunge Mwakilishi wa Kiambu Gathoni Wamuchomba wakisema vifaa hivyo ni duni na vya thamani ya chini kuliko inavyodaiwa.
Kupitia barua waliyoandikia ofisi ya Bi Muchomba, muungano huo kupitia Mwenyekiti wake Kennedy Lumbasi ulisema wanachama wake hawatachukua vifaa hivyo vinavyoendelea kuhifadhiwa kwenye ofisi ya mbunge huyo.
Walidai kuwa wanapokezwa mashine ya kukausha nywele kwa Sh10,000 badala ya Sh8,000 na kinyozi kwa Sh3,500 badala ya Sh2,000 na vifaa vingine kwa bei ya juu kuliko ya kawaida.
Sababu ya pili ya kukataa vifaa hivyo ni kubadilishwa kwa uamuzi wa awali ambao ungewawezesha kupokea vifaa hivyo bure badala ya kwa mkopo jinsi ilivyobainika baadaye.
Hata hivyo, Bi Muchomba amewalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kuutia doa mradi huo kutokana na uhasama wa kisiasa.