Habari Mseto

Madaktari waliosababisha wajawazito kupoteza watoto motoni

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Vitalis Kimutai

MADAKTARI na wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Longisa Bomet, wamekashifiwa baada ya kudaiwa kutelekeza kina mama tisa wajawazito na kupelekea wapoteze watoto wao wakijifungua.

Jamaa za kina mama hao walisema madaktari hawakuwepo kuwasaidia kina mama hao kujifungua hospitalini Ijumaa usiku hadi Jumamosi asubuhi.

Akizungumza kwa niaba ya familia zilizoathirika, Bw Edwin Bii alisema madaktari wameshindwa kuwaeleza kwa nini kina mama hao walipuuzwa jinsi hiyo. “Tumewauliza maswali lakini hakuna anayetupatia majibu badala yake wana dharau na matusi,” akasema.

Bw Bii ambaye ni kakake mmoja wa kina mama hao.

Hata hivyo, msimamizi wa matibabu katika hospitali hiyo, Dkt Isaac Birechi, alipuuzilia mbali madai hayo na kusema kuna rekodi zinazoonyesha jinsi uzalishaji ulivyofanywa na madaktari usiku huo.

“Inasikitisha kuwa kina mama wanne waja wazito waliletwa hospitalini kutoka manyumbani mwao wakiwa na matatizo ya uja uzito. Mmoja wao alitoweka hospitalini hadi Jumamosi saa kumi na mbili asubuhi,” akasema Dkt Birechi.

Hata hivyo, Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Dkt Joseph Sitonik, jana alisema ripoti kamili kuhusu madai hayo itatolewa baada ya Afisa Mkuu wa Matibabu katika kaunti kukamilisha uchunguzi wake.