Habari Mseto

Walioasi ukeketaji wahitimu

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na ALEX NJERU

WASICHANA 340 waliokataa kukeketwa msimu huu kutoka eneobunge la Tharaka hapo Jumapili walihitimu baada ya kupitia mafunzo mbadala kwa muda wa wiki moja.

Mafunzo hayo yalipangwa na kikundi kisicho cha kiserikali cha Women Welfare Program kinachopigania haki za wasichana na wanawake eneo hilo.

Wasichana wengi wenye umri kati ya miaka 10 na 17 kutoka eneo hilo hulazimishwa na wazazi na ndugu zao kutahiri kisiri wanapofunga shule kinyume na jitihada za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopinga utamaduni huo potovu.

Wakizungumza wakati wa sherehe iliyofanyika katika shule ya Msingi ya Marimanti, viongozi walisema kuna umuhimu wa kukomesha tohara za wasichana, mimba za mapema, ndoa za mapema na kubakwa kwa wasichana wadogo.

Mratibu wa chama hicho, Bi Anicenta Kiriga alisema wazazi wengine wanaendelea kutahiri wasichana wao kwa siri wakati wa usiku ili kuepuka kukamatwa.

“Tunawahimiza wazazi wetu na jamii kwa jumla kuepuka ukeketaji wa wasichana na kukumbatia mambo ambayo yanawafaidi kama vile elimu,” alisema Bi Kiriga.

Mwakilishi wadi mteule anayewakilisha jinsia katika bunge la kaunti ya Tharaka-Nithi Bi Millicent Mugana alisema kuna haja ya kuanzisha mafunzo ambayo yatachukua nafasi ya tohara ya msichana ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu.

Alibainisha kuwa imekuwa vigumu kukomesha tohara za wasichana katika jamii nyingi nchini kwa sababu jamii hazipewi tamaduni mbadala ambazo hazina shida kwa msichana.

“Tunafaa kukomesha ukeketaji wa wasichana lakini pia tunafaa kupatia jamii sherehe au mafunzo mbadala kwa wasichana,” alisema Bi Mugana.

Aidha alipendekeza kuwa sherehe hizi mbadala zinafaa kufanyiwa vijijini wala si shuleni, makanisani au mijini ili kuwahusiacha wanakijiji jinsi ilivyokuwa na ukeketaji.

Mwakilishi wadi ya Marimanti Bi Susan Ngugi alisema kuwa imekuwa ngumu kukomesha tohara kwa wasichana kwa sababu serikali na vikundi visivyo vya kiserikali vimelenga tu wasichana huku wanajamii wengine wakiachwa kwa giza.

“Tumewapa mwanga wasichana na kuwaacha wazazi na jamii kwa jumla ambayo inawalazimisha kukeketwa,” alisema Bi Ngugi.

Wiki mbili zilizopita, mama wawili walifungwa miaka saba gerezani na koti ya Maimanti na mwingine kufungwa miaka sita na koti ya Chuka kwa kupatikana na makosa ya kulazimisha wasichana wao kukeketwa.