OBARA: Jopo la kuchunguza makosa vitabuni liokoe watoto wetu
Na VALENTINE OBARA
INATIA moyo kusikia kwamba hatimaye serikali imechukua hatua kwa lengo la kuboresha yaliyomo kwenye vitabu vinavyotumiwa katika shule zetu.
Kwa miaka michache sasa, mashirika ya habari yamekuwa yakiangazia jinsi baadhi ya vitabu vilivyosambazwa na serikali kwa shule za msingi na upili vilivyojaa makosa, gazeti la Taifa Leo likiongoza katika ufichuzi wa suala hili.
Walimu hulalamika kimyakimya kuhusu makosa yaliyomo vitabuni kwani wengi wao huhofia kuadhibiwa na mwajiri wao ambaye ni serikali endapo watapaza sauti. Lakini kwa bahati nzuri, wananchi kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa kwenye mstari wa mbele kufichua makosa haya.
Licha ya ufichuzi uliokuwa ukifanywa kwa muda huu wote, hasa tangu serikali ilipoharakisha kusambaza vitabu bila malipo kwa shule za umma, hakujakuwa na hatua yoyote ya kuridhisha hadi wiki iliyopita.
Kwa kuunda jopokazi ambalo lina jukumu la kuchunguza vitabu vilivyoidhinishwa na Taasisi ya Uundaji wa Mtaala Kenya (KICD), natumai kwamba Waziri wa Elimu Amina Mohamed ana nia njema ya kutafuta suluhisho la kudumu.
Imekuwa ikisikitisha jinsi kila mara kunapofichuliwa kwamba kuna vitabu vya shule vyenye kasoro, wachapishaji hujitokeza kwa haraka kujitetea bila kutueleza kile wanachopanga kufanya kuzuia makosa hayo yasirudiwe au hata wanachofanya kurekebisha makosa hayo.
Wadau hawa hawana huruma kwa watoto maskini ambao ndio hutegemea zaidi vitabu hivi vya serikali.
Shule za mijini
Ninasema hivi kwa kuwa katika mahojiano yangu na walimu mbalimbali, niligundua kuwa walimu katika shule za mijini hufanikiwa kuwashawishi wazazi kununua vitabu mbadala ambavyo huwasaidia masomoni badala ya kutegemea vile vilivyo na makosa.
Hii ina maana kuwa watoto wanaotoka katika familia maskini zisizo na uwezo wa kugharamia vitabu vingine husalia kutegemea ushauri wa walimu wao pekee ambao pengine watawasaidia kukosoa sehemu za vitabu walivyo navyo.
Uamuzi wa Wizara ya Elimu kuunda jopokazi la kuchanganua vitabu kuanzia chekechea hadi darasa la tatu ambavyo naamini ni vya mtaala mpya, ni hatua ya kwanza tu.
Hii isiwe kama majopokazi ya awali ambayo ripoti zao ziliishia kuhifadhiwa katika sehemu zisizojulikana baada ya wanajopo kumumunya hela tele za mlipaushuru katika uchunguzi wao.
Ingawa tunafahamu tatizo kwenye vitabu liko hadi shule za upili, natumai uchunguzi utakaofanywa kwa madarasa haya ya chini yaliyoanza kutekeleza mtaala mpya utatoa mwongozo kuhusu kinachohitaji kufanywa ili kuhakikisha watoto wetu hawapotoshwi.
Iwapo tatizo ni la wachapishaji vitabu, serikali isisite kufanya uamuzi unaostahili ikiwemo kuwazuia wachapishaji waliozembea katika majukumu yao.
Vile vile, iwapo itapatikana kuwa tatizo li kwenye taasisi husika za serikali, kuna sheria za kitaifa na sera za serikali zinazopaswa kutumiwa kikamilifu kuwaadhibu maafisa watakaobainika hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo.