• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
MOKAYA: Man City ikipigwa tena, yake kwisha

MOKAYA: Man City ikipigwa tena, yake kwisha

NA JOB MOKAYA

KUNA msemo wa Uswahilini usemao kwamba kaa akiinua gando yamekatika. Kaa ni mnyama wa baharini mwenye gando au sehemu ngumu kama chuma inayofunika mwili wake kwa nje ili kujilinda.

Anaposhambuliwa, ni mwepesi wa kutumia gando lake kujificha hadi adui yake apite ndipo apate kujitokeza tena kama afanyavyo kobe.

Timu ya Manchester City ilipokea kichapo kwenye ligi kuu ya Uingereza kwa mara ya kwanza kabisa siku ya Jumamosi baada ya kulambishwa mabao mawili bila jawabu lolote kutoka kwa Chelsea, ngoma iliyochezwa Stamford Bridge.

Kichapo hiki cha City kiliwateremsha ardhini kutoka mbinguni ambako wamekuwa wakielea kwa muda sasa. Kabla ya mechi hii, wachanganuzi wengi wa soka walikuwa wamehoji kwamba City ingaliiadhibu Chelsea bila huruma wowote lakini mambo yakaenda kinyume sana na matarajio ya wengi.

Hali ina maana kwamba timu ya Liverpool imechukua uongozi wa ligi kuu ikiwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 16 huku ikifuatwa na Manchester City kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 41. Tottenham ni ya tatu kwa pointi 36 nazo Chelsea na Arsenal zinafunga tano zikiwa na pointi 34 lakini Arsenal inadunishwa na mabao. Manchester United ni ya sita.

Endapo Manchester City itapoteza mechi nyingine nayo Liverpool kushinda, basi pengo kati yake na Livepool litakuwa alama 4 kwa dhana kwamba nayo Liverpool haitapoteza mechi.

La muhimu ni kwamba, endapo City watapoteza mechi nyingine basi kujiamini kwao kutakuwa kumeporomoka nao wataanza kupoteza mechi moja baada ya nyingine.

Matokeo yake yatakuwa Liverpool kushinda ligi kwa mara ya kwanza baada ya miongo mingi naye Pep Guardiola kuwekwa kwenye nafasi yake ambapo atakuwa anang’ang’ania nafasi ya nne bora wenzake wakiwa Arsenal na Manchester United.

Manchester City wamekuwa wakicheza mchezo mzuri sana hususan kwenye ligi na kushinda mechi nyingi mno. Ni kushinda huko ambako kumewafanya kuogopwa na wengi na hivyo kuwatia wapinzani hofu ya kisaikolojia. Hofu hiyo sasa imeanza kutoweka nayo itapotea kabisa wakati City itapokezwa kichapo kingine.

Mabao ya Chelsea yalifunga na kiungo cha kati Nkolo Kante kunako dakika ya 45 kipindi cha kwanza, nalo bao la pili lilitiwa kimiani naye difenda David Luiz kunako dakika ya 78 ya mchezo. Licha ya City kutapatapa hapa na pale, hawakuweza kupata angalau bao la kufutia machozi.

Manchester City wanarudi tena dimbani kesho kutwa (Jumatano) kwenye mtanange wa Champions League ambapo watachuana na Hoffenheim ya Ujerumani katika uga wao wa nyumbani wa Etihad.

Tayari City imefuzu kwenye awamu ya mwondoano ya Champions League huku ikikalia uongozi wa kundi lake ambalo linahusisha Olympique Lyon, Shakhtar Donetsk na hiyo Hoffenheim.

Baada ya michuano ya katikati ya juma ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, City itatua tena dimbani siku ya Jumamosi kuzichapa na Everton katika uga wa Etihad.

Mechi hiyo itaanza saa tisa unusu alasiri.Bila ya shaka yoyote, mtu aliyekuwa na furaha riboribo kutokana na ushinde wa City ni Liverpool. Timu zote zilizo katika sita bora zilishinda mechi zao za wikendi isipokuwa Manchester City.

Liverpool iliishinda Bournemouth kwa mabao 4-0; Arsenal ikailima Huddersfield Town kwa bao moja kwa yai nayo Manchester United ikaiangusha Fulham kwa mabao manne kwa moja. Tottenham ilifunga siku kwa kuishinda Leicester kwa mabao mawili kwa bila.

You can share this post!

Mbappe kumtwaa rasmi kimwana Alicia Aylies

Mwanzo wa mwisho wa Messi na Ronaldo

adminleo