• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
UKEKETAJI: Uvumbuzi wa wasichana Wakenya kuokoa ulimwengu

UKEKETAJI: Uvumbuzi wa wasichana Wakenya kuokoa ulimwengu

NA FAUSTINE NGILA

KENYA inazidi kushuhudia akili pevu zenye mawazo bora ya uvumbuzi wa kidijitali ambayo yamechangia pakubwa katika uchumi wa nchi na kurahisisha jinsi baadhi ya changamoto katika jamii zinakabiliwa.

Katika sekta za fedha, utalii, elimu, uchukuzi, mawasiliano, kilimo na afya utapata programu za simu ambazo zimeundwa na Wakenya, na zinazotumika hata katika mataifa ya nje.

Taifa hili lenye intaneti ya kasi ya juu zaidi duniani, pamoja na asilimia kubwa zaidi Afrika ya wananchi wanaomiliki simu za kisasa almaarufu smartphones, ni jiko la kuandaa baadhi ya programu zinazotikisa dunia.

Uvumbuzi wa hivi majuzi umetoka Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu, ambapo wasichana watano wameungana kuunda programu ya simu inayosaidia pakubwa akukabiliana na ukeketaji. Hii ni licha ya uvumbuzi humu nchini na hata duniani kote kutawaliwa na wavulana na wanaume.

Wasichana hao Purity Achieng, Macrine Atieno, Synthia Otieno, Stacy Owino na Ivy Akinyi wameibuka washindi wa mwaka huu wa Tuzo ya Mwafrika wa Mwaka inayoandaliwa na shirika habari la Daily Trust kutoka Nigeria.

Mabinti hao wameunda ‘apu’ kwa jina I-cut ambayo walisema itasaidia kuwaunganisha wasichana wote waliolazimishwa kukeketwa, na kuwapa usaidizi wa kisheria na kimatibabu.

Vipusa hao wanaojiita “the Restorers” ni kundi la kwanza kutoka humu nchini kushinda tuzo hiyo ya Sh2.5 milioni.

Wasichana wanaolazimishwa kukeketwa wataweza kutumia programu hiyo ya simu kuwaarifu maafisa husika kwa kubonyeza kitufe na kuweza kuokolewa.

Kulingana na tovuti ya Daily Trust, wasichana hao watano watatuzwa katika sherehe itakayoandaliwa jijini Abuja hapo Januari 2019, ambapo watapokea kitita chao cha Sh2.5 milioni.

“Programu hiyo imeanza kuwa silaha muhimu katika vita dhidi ya ukeketaji,” taarifa kutoka kwa Kamati ya Uteuzi wa tuzo hiyo ilisema.

Kamati hiyo inaongozwa na aliyekuwa rais wa Botswana, Festus Mogae.

I-cut ni programu ya kisasa inayounganisha wasichana walio kwa hatari ya kukeketwa na vituo vya usaidizi na uokoaji. Inawapeleka waathiriwa hospitalini na kuwapa mawakili wa haki za kibinadamu katika juhudi za kukomesha uovu huo.

“The Restorers” wanashirikiana na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali katika wajibu wake wa kutokomeza ukeketaji wa wasichana.

Kundi hilo liliwabwaga Wakenya tisa waliokuwa katika mchujo wa mwisho na kujipatia nafasi katika shindano la Technovation Challenge liliandaliwa mwezi Agosti mwaka huu katika jimbo la California, Amerika.

Walikutana na washindani wengine kutoka mataifa mengine duniani. Yakidhaminiwa na kampuni za Google, Salesforce na Adobe, mashindano ya hayo teknolojia huwarai wasichana wa miaka kati ya 10 na 18 kuunda programu ambayo inasuluhisha matatizo ya kijamii.

Katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Hazina ya Masuala ya kidharura ya Watoto (UNICEF), kuhusu utafiti wa mataifa 29 barani Afrika na Mashariki ya Kati, Ethiopia ilitajwa kuwa na idadi kubwa zaidi duniani ya wasichana na wanawake waliokeketwa (27.2 milioni).

Kutokana na uhamiaji, ukeketaji umesambaa katika kila pembe ya dunia, huku baadhi ya familia zikiwataka mabinti zao kukeketwa wakati wakiwa likizoni katika mataifa ya kigeni.

Huku serikali nyingi duniani zikizidi kupambana na dhuluma hii dhidi ya wasichana, sheria zimebuniwa kuhakikisha wanaopatikana na hatia wamehukumiwa mahakamani.

Mnamo mwaka 2006, Khalid Adem aliweka historia kwa kuwa mwanamume wa kwanza nchini Amerika kuhukumiwa gerezani kwa kumkeketa bintiye.

Humu nchini, ukeketaji unafanyika zaidi katika kaunti za Kaskazini Mashariki (97.5%), %), Nyanza (32.4%), Rift Valley (26.9%), na Mashariki (26.4%), huku asilimia ya chini ikiwa katika kaunti ya mikoa ya Kati (16.5%), Pwani (10.2%), Nairobi (8.0%), na Magharibi (0.8%).

Jamii ambazo kufikia sasa bado zinashikilia utamaduni wa tohara ya wasichana ni Wasomali (93.6%), Wasamburu (86.0%), Wakisii (84.4%) na Wamasai (77.9%). Takwimu hizi ni kulingana na utafiti uliofannywa na Wizara ya Afya hapo mwaka 2014.

Wakati Umoja wa Mataifa ukijizatiti kumaliza mtindo huu kufikia mwaka 2030, wavumbuzi wamekuwa wakipewa motisha kuvumbua teknolojia ambazo zitasaidia kukomesha ukeketaji, hasa barani Afrika na Uarabuni ambapo utamaduni umechangia pakubwa kuendeleza uovu huo.

Na uvumbuzi wa ‘The Restorers’ unatazamiwa kuokoa ulimwengu mzima kutokana na minyororo ya ukeketaji.

You can share this post!

SIAYA: Matumaini tele kwa wakazi baada ya dhahabu...

#HonoluluMarathon: Wakenya wavuna mamilioni

adminleo