• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
AKILIMALI: Mafunzo muhimu kwenye warsha ya kilimo na ufugaji

AKILIMALI: Mafunzo muhimu kwenye warsha ya kilimo na ufugaji

NA FAUSTINE NGILA

KIU ya wakulima kuelewa mbinu bora za ukuzaji wa mimea na ufugaji wa mifugo inazidi kupanda katika maeneo mengi humu nchini.

Hilo lilidhihirika hapo Novemba 10, wakati Akilimali ilitua kaunti ya Narok Narok na kushiriki katika warsha ya mafunzo kwa wakulima ya Seeds of Gold, jarida linalochapishwa na Saturday Nation.

Kilomita moja kutoka mjini Narok, katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, kampuni za vifaa na bidhaa za kilimo, wakulima, wataalamu na wanafunzi wa chuo hicho walikongamana kujadili jinsi ya kuboresha kilimo.

Mtaalamu wa kilimo cha mimea wa Chuo Kikuu cha Egerton Bi Carol Mutua ajibu maswali kuhusu kilimo cha viazi. Picha/ Faustine Ngila

CMC Motors, Elgon Kenya, Kienyeji Kenya, Chuo Kikuu cha Egerton, Idara ya Kilimo ya kaunti ya Narok, Taasisi ya Mafunzo ya Sensei, Coopers Kenya, Car & General, ATSL ni baadhi ya kampuni zilizofika na wataalamu kujibu maswali ya wakulima waliotoka kaunti za Narok, Nakuru, Nairobi, Kiambu, Kericho na Bomet.

Mtaalamu wa mimea katika Chuo Kikuu cha Egerton Benard Towett alianza kwa kuwashauri wakulima kununua aina mpya za mbegu za maharagwe, mtama na ngano ambazo zimeundwa kimahususi kwa kaunti ya Narok.

“Maharagwe ya Chelalang yana faida mno. Ukiwekeza Sh30,000 utazoa Sh90,000. Baada ya kuwapa mbegu za mtama, tutawaunganisha wakulima na kampuni za kuunda pombe,” akasema.

Mtaalamu wa ufugaji kuku Dkt Subiri Obwogo (kushoto) ajibu maswali ya wafugaji. Picha/ Faustine Ngila

Mkulima aliyejitambulisha kama Priscah alielezea tabu wanayopata wakulima kupata mbegu halisi za viazi. “Pata mbegu zilizoidhinishwa katika kituo cha ATC Molo au Kisima, Meru,” alijibiwa na mhadhiri wa kilimo Bi Carol Mutua, kutoka Chuo Kikuu cha Egerton.

Ilikuwa furaha kwa wakulima wa Narok kujuzwa kuwa kuna mbegu za aina mpya ya wimbi, zinazochukua muda mfupi wa siku 75 kukomaa.

Hata hivyo, wakulima wote walionywa dhidi ya kupanda mmea mmoja kila msimu katika eneo moja la shamba. Walitakiwa kupanda maharagwe kwa msimu unaofuata ili kupunguza kiwango cha asidi mchangani na kurutubisha shamba.

Mtaalamu ajibu maswali ya wanafunzi kwenye kibanda chake. Picha/ Faustine Ngila

Mwanajeshi Ken Kasura alitaka aelezwe kuhusu mbinu mwafaka ya kujiundia lishe ya ng’ombe wa maziwa.

Mtaalamu John Muchibi kutoka Elgon Kenya alianza kwa kusema kuwa hakuna mbinu mahsusi ya kuunda lishe.

“Mbinu ya kuunda lishe hutegemea afya ya mifugo, idadi, umri na mahitaji ya madini mwilini. Ingawa kuna programu ya kompyuta ya kuweka vipimo mwafaka vya viambato hitajika, lazima kwanza uelewe mifugo wako,” akasema.

Naye mkali wa lishe kutoka Coopers Kenya Bw Edwin Too alionya kuwa ingawa mfugaji anaweza kuunda lishe bora, iwapo atakosea kuhusu jinsi ya kuwapa mifugo lishe hiyo, basi tatizo lile litasalia tu.

Mhadhiri wa kilimo katika Chuo Kikuu cha Egerton Bw Felix Akatch alipowaonya wafugaji dhidi ya kuuza maziwa yenye ugonjwa wa mastitis. Picha/ Faustine Ngila

Bw Muchibi aliwashauri wakulima kuunda vikundi vya kutengeneza lishe ya mifugo kwa kuwa viambato vyake ni ghali, akiongeza kuwa hiyo itasaidia kuunda lishe kwa mbinu inayofaa.

Mfugaji mmoja aliomba kujua sababu ya ng’ombe wake aliyemnunua Murang’a kukosa kumpa maziwa aliyotarajia alipomfikisha Narok.

“Kuna aina tofauti za ng’ombe kwa maeneo tofauti ya hali ya hewa. Ng’ombe uliyemtoa kwa maeneo ya milimani kumleta meneo ya chini hawezi kutimiza matarajio yako kwa kuwa maji hubadilika na viambato vya lishe unayompa ni tofauti kwa kuwa mchanga umebadilika,” akajibu Bw Muchibi.

“Mbona ng’ombe wangu aliyekuwa ananipa lita 35 za maziwa kwa siku sasa hafikishi lita 30 na hajazeeka?” aliuliza mfugaji mmoja.

Mtaalamu wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa John Muchibi ajibu maswali tata ya wakulima. Picha/ Faustine Ngila

Alijibiwa kuwa sababu kuu ni kuwa ng’ombe huyo anaugua ugonjwa wa kugandisha au kutia damu kwa maziwa almaarufu mastitis ambao hauonekani.

“Kuna aina mbili za ugonjwa huu, ule unaoonekana na ule uliojificha. Uliojificha ni hatari zaidi kwa kuwa huwezi kutambua na ni rahisi kuambukiza ng’ombe wengine ukiamini ng’ombe wako yu buheri wa afya.”

Walitakiwa kutumia kikombe cha kitaalamu na kukama tone moja la maziwa na kuona iwapo kuna rangi inayokaribia wekundu.

Dkt Enock Ng’eno kutoka Coopers Kenya alisema iwapo ng’ombe ataugua ugonjwa huo, kiwango cha maziwa kitapungua kabisa.

Kampuni ya CMC Motors ilipamba warsha hiyo kwa trakta zake za kisasa za kilimo aina ya New Holland. Picha/ Faustine Ngila

“Mwite mtaalamu wa ng’ombe aliyetimu ambaye atapeleka maziwa yako kwa maabara na kutambua kiini cha ugonjwa huo. Sitisha kumkama hadi pale atakwambia uendelee. Tumia mafuta ya kukama aina ya mastrite kuosha matiti. Ugonjwa huu huua,” alisema.

Wakati mwingine mafuta ya kukama huenda ndicho chanzo cha ugonjwa huo, hasa iwapo mfugaji anatumia kitambaa kimoja kupangusa matiti ya ng’ombe wote anaokama kwa kuwa kinanasa bakteria. Kila ng’ombe anafaa kutengewa taulo yake binafsi.

Maafisa wa CMC Motors wakikagua majawapoa ya trakta za kisasa. Picha/ Faustine Ngila

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Egerton Felix Akatch alisema kuwa ugonjwa wa mastitis unfaaa kuzuiwa kwa njia zote kwa kuwa maziwa ni chakula cha binadamu. “Inasikitisha kuwa baadhi ya wafugaji huuza maziwa yenye ugonjwa huu,” alisema.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara aliuliza sababu ya kupe kuzidi kuwauma ng’ombe licha ya kusharaziwa dawa ya kuwaua.

Bw Muchibi alimjibu kuwa kiini ni utumizi wa dawa moja kila wakati. “Unafaa kutumia dawa tofauti kila wakati. Lenga masikio, kwato na mkia na ufanye hivyo kila wiki. Hakikisha umesharaza dawa hiyo kutoka upande wa nyumba ili iinue manyonya na kufikia ngozini ambapo kupe wadogo hujificha.”

Bi Lucy Muia wa kampuni ya CMC Motors aonyesha mojawapoa ya trakta nyingi kampuni hiyo inayouzia wakulima kuboresha mavuno. Picha/ Faustine Ngila

Mwanafunzi mwingine aliuliza mbinu atakayotumia kugeuza ng’ombe wake wa zebu kuwa wa kisasa ili amletee maziwa mengi.

Alijibiwa kuwa mwanzo ahakikishe kuwa ng’ombe wake huyo hana magonjwa kisha asake fahali wa aina ya Boran wakati anahitaji ndume. Lazima fahali huyo awe amesajiliwa.

Pia alishauriwa kutumia mbinu ya kuzalisha ya kiteknolojia ya AI lakini ahakikishe shahawa anazonunua ni zile zilizoundwa kuzaa ndama wa kike, ili kizazi kiboreke haraka. Ndama huyo akikomaa na kufikisha uzani wa kuzaa, alishauriwa kumtia shahawa za Friesian.

Mkulima auliza wataalamu swali. Picha/ Faustine Ngila

Mfugaji mwingine alitaka kujua sababu ya manyoya ya ng’ombe wake wa Friesian kugeuza rangi na kuwa ya kikahawia na kuavya mimba kila ujauzito unapofikisha miezi sita.

“Hiyo inaonyesha ng’ombe wako amekosa madini ya copper kwenye lishe unayompa. Mchanga wa shamba unakokuza lishe hiyo umejaa madini ya iron na kufanya copper kukosekana. Pia uwepo wa aflatoxin kwenye lishe hubadilisha rangi.”

Mtaalamu wa kilimo wa Chuo Kikuu cha Egerton Bw Felix Akatch amwelzea mwenzake kuhusu trakta la kisasa la kampuni ya CMC Motors kwenye warsha iliyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara. Picha/ Faustine Ngila

“Uavyaji wa mimba kwa mifugo hutokana na bakteria za brucella. Pia inawezekana shahawa ulizompa ng’ombe zilikuwa na maambukizi ya magonjwa. Ndio maana unashauriwa kutumia shahawa hizo kwa ng’ombe bikira pekee,” akajibiwa.

Wakulima wa mahindi kuishangaa serikali kushusha bei ya gunia moja la mahindi hadi Sh1,200 licha ya gharama za kuzalisha gunia hilo kugonga Sh2,000, kisha warsha hiyo ikafika tamati.

You can share this post!

Wabunge kuchunguza mimba za mapema

SHERIA ZA MICHUKI: Hakuna mjadala kuhusu sheria kwa matatu

adminleo