Jaji mwanaharakati Willy Mutunga awasihi wanahabari kuwakingia mashoga
NA SINDA MATIKO
ISHU ya jamii ya mashoga na wasagaji nchini imeendelea kuibua hisia kali nchini Kenya huku ikionekana kupingwa sana na jamii, dini, wanasiasa na hata katiba ya nchi.
Hata hivyo, machoni mwake aliyekuwa Jaji Mkuu Profesa Willy Mutunga ambaye ni miongoni mwa vichwa vikubwa vilivyohusika kuandaa katiba ya sasa ya nchi, jambo hilo linapaswa kubadilika.
Akitoa hotuba wakati wa chakula cha jioni katika sherehe ya funga mwaka iliyoandaliwa na waandishi wa burudani, sanaa na utamaduni nchini Entertainment and Arts Journalists Association of Kenya (EAJAK), mstaafu jaji aliwaza tofauti kuhusiana na ishu hiyo ya mashoga nchini.
“Katiba inawaruhusu nyie wanahabari kuangazia mambo mengi sana yanayoikumba jamii yetu. Mnaweza mkaangazia masuala ya raslimali, itikadi na imani, tamaduni zetu, manyanyaso na mengine kibao endapo hamtazuiwa kufanya hivyo. Nyie wanachama wa EAJAK mnapaswa kuwa wanaharakati kwenye mambo haya, sioni kwa nini mwogope. Mumeishi kwa kusua ila kwa mtazamo wangu mnapaswa kuhusuka,” profesa alitanguliza.
Na kisha akaendelea,
“Kuna hoja nyingi zimeibuliwa zinazotajwa kuwa tatanishi ila sioni ni kwa nini msiangazie. Hakuna hoja tatanishi kwa mwanahabari. Kwa mfano ishu ya jamii ya LGBTQIA+ kumekuwepo na malumbano kadhaa ila hakuna mtu anayetaka kuitathmini ishu hiyo kwa undani kuona ni nini sawa na kipi sio sawa. Kuna taasubi fulani ya wanahabari kupenda kukwepa kuangazia hoja tatanishi kama hizi, nasisitiza mnapaswa kubadilika.”
Ikumbukwe tu kwamba Mutunga 76, aliwahi kuzua tetesi kuwa yeye ni shoga kati ya 2011 na 2016 alipohudumu kama Jaji Mkuu kutokana na yeye kupenda kuvalia herini kwenye sikio lake moja.
Juzi kati kwenye mojawepo ya mahojiano aliyoyafanya na Business Daily, Jaji Mutunga aliangazia sakata hiyo tena na kusema sababu yake ya kuvalia herini ilitokana na mwito wa wazee wake ikiwa ni sehemu ya tambiko ili kuwafurahisha mababu zake.