Maina Njenga aonywa dhidi ya kujaribu kufufua Mungiki
NA WANDERI KAMAU
MMOJA wa viongozi wa zamani wa kundi la Mungiki, Bw Ndura Waruinge, amemuonya mwenzake, Bw Maina Njenga, dhidi ya kujaribu kuvuruga hali ya amani nchini.
Bw Waruinge, ambaye sasa ni mhubiri, alimwambia Bw Njenga kujiepusha na vitendo vyovyote ambavyo huenda vikasababisha umwagikaji damu.
“Bw Maina Njenga ni binamu yangu; tulikuwa viongozi wakuu katika kundi la Mungiki. Hata hivyo, ningetaka kumshauri aende pole pole. Kenya inahitaji kila mmoja; tunahitajiana sisi sote.
Usiwahi kufanya jambo lolote linaloweza kuzua ghasia nchini. Kenya ni ya kila mmoja, hata ikiwa humpendi Rais. Sote tu Wakenya,” akasema Bw Waruinge.
Mhubiri huyo alisema kuwa Kenya haiwezi kurudi nyuma kutokana na hatua ilizopiga katika kufikia amani na umoja uliopo.
Wawili hao ndio walianzisha kundi hilo haramu.
Kauli yake ilijiri siku moja baada ya maafisa wa usalama kuzima mkutano uliopangiwa kuongozwa na Bw Njenga katika uwanja wa Kabiru-ini, mjini Nyeri, mnamo Jumapili.
Zaidi ya watu 250 wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi hilo walikamatwa na polisi kwenye msako ulioendeshwa katika sehemu tofauti nchini.
Kamishna wa Kaunti ya Nyeri, Bw Pius Murugu, alitoa agizo la kupigwa marufuku kwa mkutano huo Jumamosi.
Bw Murugu alitoa agizo kwa vikosi vya usalama na viongozi wa Nyumba Kumi kusimamisha mikutano ya aina yoyote ile katika maeneo wanakosimamia.
“Hatutaruhusu mkutano huo katika eneo hili. Nyeri imekuwa ni kaunti yenye amani. Tunawaonya wale wote wanaojaribu kufufua kundi hilo kwamba watakabiliwa vikali,” akasema Bw Murugu.
Bw Njenga alikuwa amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni “kubuni mwelekeo wa kisasa wa eneo la Mlima Kenya”.