Habari Mseto

Awinja: Kutuzwa na Rais haimaanishi nimeingia kwenye siasa

January 2nd, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

MVUNJA mbavu Jacky Vyke almaarufu Awinja ameamua kunyoosha baadhi ya tetesi ambazo zimeibuka toka alipotuzwa na  Rais William Ruto.

Kwenye sherehe za Jamuhuri Dei 2023, Awinja alikuwa miongoni mwa wanasanaa wachache walioheshimishwa kwa kutunukiwa tuzo za kitaifa kiwango cha Order Of The Grand Warrior (OGW)  ikiwa ni utambuzi wa mchango wake kwenye tasnia ya sanaa.

Lakini wapo baadhi ya mashabiki wake ambao wamehoji kwamba kuheshimishwa huko huenda ukawa pia ni njia ya Awinja kuvutuwa kujitosa kwenye uchaguzi jinsi ambavyo imekuwa ikishuhudiwa na maceleb kibao.

Hata hivyo, mrembo huyo anasema hana muda na siasa na wala hajawazia kuingia kwenye siasa.

“Sina nia wala matamanio ya kujitosa kwenye siasa, hayo sio mawazo sahihi. Naamini kuheshimishwa kwangu na Rais kumetokana na mchango wangu kwenye tasnia ya burudani. Kwamba nimekuwa nikiwaburudisha Wakenya kwa miaka sasa na wengi wameridhia. Huo ndio mkakati ninaopanga kuendelea nao na wala si vinginevyo,” Awinja kakata kauli.

Aidha, msupa huyo kasisitiza kuwa kazi ya burudani anayoifanya haifanyi kwa ajili ya kupata tuzo.

“Tunachokifanya sio kwa sababu ya msukumo wa kutuzwa ila ni kwa sababu tunapenda kufanya tukifanyacho. Lakini pia kama tuzo na kuheshimishwa zikitokea kwa sababu za kazi zetu hizi, basi ile ni nyongeza na tunashukuru kutambuliwa maana ni hakikisho kuwa tunachokifanya ni kitu kizuri.”