Mwanzilishi wa ‘Ondoa Panya’ kukumbukwa kwa kumtetea mnyonge
NA WANDERI KAMAU
CHAMA cha Safina, ambacho kinaongozwa na wakili na mwanasiasa mkongwe, Bw Paul Muite, kimempoteza Katibu Mkuu wake.
Bw John Wamagata, ambaye ni wakili, alifariki Jumatano wiki iliyopita na atazikwa hapo Ijumaa, Januari 5, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa chama hicho, Bw David Wanjohi, alisema kuwa familia ya marehemu ilikubaliana mazishi hayo kufanyika Ijumaa.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Wanjohi alisema kuwa ibada kabla ya mazishi itafanyika katika Shule ya Msingi ya Kinoo, eneobunge la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, ambapo baadaye atazikwa nyumbani kwake, karibu na shule hiyo.
Bw Wanjohi alisema kuwa chama hicho kimempoteza kiongozi shupavu, aliyejitolea kutetea haki za raia.
“Tumempoteza kiongozi shujaa ambaye hakupenda watu wenye mzaha,” akasena Bw Wanjohi.
Mnamo 2020, Bw Wamagata alianza kampeni kali iitwayo ‘Ondoa Panya’, iliyolenga kuwaondoa madiwani wafisadi katika mabunge ya kaunti.
Bw Wamagata alishikilia kwamba madiwani walikuwa wamezigeuza serikali za kaunti kuwa majukwaa ya kujitajirisha, badala ya kuwaletea maendeleo raia.
Aliwafananisha madiwani na panya, ambao hula kila kitu bila kubakisha chochote.
“Madiwani tulio nao wanafanana na panya. Hawajali maslahi ya raia, bali lengo lao ni kujitajirisha. Ikiwa hii ndiyo ilikuwa maana kamili ya ugatuzi, basi tutawaondoa wote kutoka mabunge ya kaunti ili kuwakomboa raia kutokana na ulafi wao,” akasema Wamagata wakati akiwa hai.