Kimataifa

Ndege zagongana na kuua watu sita

January 3rd, 2024 1 min read

Na MASHIRIKA

NDEGE moja iliyokuwa imebeba abiria ililipuka moto Jumanne katika uwanja wa ndege wa Haneda jijini Tokyo, Japan baada ya kugongana na ndege ya walinda usalama wa baharini.

Ndege hizo ziligongana kwenye mkondo wa ndege kukimbilia kabla ya kupaa.

Abiria wote 379, wakiwemo watoto wanane, na wahudumu waliokuwa ndani ya ndege hiyo nambari Flight 516 walinusurika katika kile kilichotajwa kama “muujiza”.

Hata hivyo, watu sita waliokuwa ndani ya ndege ya walinda usalama wa baharini na wahudumu walipatikana wamekufa huku rubani akinusurika.

Ndimi za moto zilionekana zikifuka kutoka kwa madirisha ya ndege hiyo aina ya Airbus A-350 ilipokimbia kwenye lami baada ya kutua.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, ambaye tayari anashughulikia madhara ya tetemeko la ardhi nchini humo, alituma rambirambi zake kwa familia za waliokufa.