Koome amjibu Ruto: Ikiwa una ushahidi wa majaji fisadi upeleke JSC
NA FATUMA BARIKI
Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) Martha Koome amemjibu Rais William Ruto kuhusu madai kwamba majaji ‘wafisadi’ wanatoa maamuzi ya kupinga miradi yake ya maendeleo.
Kupitia taarifa kwa umma, Januari 3, 2024, Jaji Mkuu anaelezea kusikitishwa kwake na kile alichosema ni mtindo wa maafisa wa serikali na watumishi wa umma kushambulia Idara ya Mahakama pindi maamuzi yanapotolewa na kuonekana kwenda kinyume na matarajio yao.
“JSC imebaini kwa masikitiko makuu kwamba majaji na maafisa wa Idara ya Mahakama wanashambuliwa kwa kutoa maamuzi ambayo yamechukuliwa kuwa ya kupinga miradi ya serikali. Tume ingependa kusisitiza kuhusu uhuru wa Mahakama kama mojawapo ya nguzo kuu za serikali ilivyonakiliwa kwenye Katiba na inawapa shime majaji na maafisa wake wote kuendelea kutekeleza majukumu yao bila woga wala mapendeleo,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais Ruto ameendelea kupata ukosoaji mkubwa kufuatia matamshi yake Januari 2 katika Kaunti ya Nyandarua ambapo alisema hataheshimu maagizo yoyote ya mahakama ambayo yatakwamisha miradi yake ya maendeleo.
Alikuwa akihutubu katika mkutano wa mazishi ya baba ya Seneta wa Nyandarua John Methu ambapo, akiongea akiwa mwingi wa hamaki, alishutumu maafisa wa mahakama kwa kile alichosema kwamba huhongwa ili kutoa maagizo ya kukwamisha sera za serikali yake.
Miongoni mwa maamuzi ya hivi punde ambayo yanaaminika Rais alikuwa akirejelea ni kusimamishwa kwa makato ya nyumba ambayo uamuzi katika Mahakama ya Rufaa unasubiriwa baadaye Januari. Mpango wake vile vile wa Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) umekumbwa na vizingiti.
Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/koome-akohoa-sasa