Demu anataka nimuoe na sina nyumba; nihamie kwake?
Kwako shangazi. Mpenzi wangu ni mwanamke anayejiweza kifedha. Anataka nimuoe lakini mimi sina nyumba. Nimemuomba anipe muda hadi nijenge lakini anasisitiza tuishi kwake. Waonaje?
Hali ya kawaida inahitaji mwanamume kuwa na kwake kabla hajaoa. Lakini kwa sasa ndoa ndilo jambo muhimu zaidi kwa mpenzi wako. Kubali ombi lake. Unaweza kujenga kwako mkiishi kwake.
Kuna mdada kanisani amefungua roho
Kwako shangazi. Nilimaliza masomo majuzi na ninatafuta kazi. Mwanamke tunayeabudu kanisa moja ameniambia ananipenda. Ana kazi nzuri na pesa na sielewi ana nia gani kwangu. Nishauri.
Si kawaida kwa mwanamke kuungama mapenzi yake kwa mwanamume. Pili, mapenzi ya dhati yana nguvu. Sidhani mwanamke huyo ana nia nyingine kwako isipokuwa tu mapenzi. Kama unampenda mpe moyo wako.
Nina wasiwasi mke bado hajanizalia mtoto
Kwako shangazi. Nilimuoa mpenzi wangu miaka mitatu iliyopita na kufikia sasa hatujapata mtoto. Mke wangu ananiomba tungoje kidogo ingawa hajanipa sababu yoyote. Nina wasiwasi. Nishauri.
Sielewi ni kwa nini mke wako ameamua kuahirisha jambo hilo. Ni muhimu uzungumze naye ujue sababu. Huenda bado hajaamua kuhusu iwapo anataka kuwa mama ya watoto wako na anashindwa kukwambia.
Mke ameanza jeuri ni kama anagawa nje
Vipi shangazi? Ninashuku mke wangu ana mpango wa kando. Ameanza kunikosea heshima na hata kuninyima haki yangu chumbani. Ninaumia moyoni, nishauri.
Huo ni mwelekeo hatari katika ndoa. Mketishe chini mke wako umkanye dhidi ya mienendo yake. Mkumbushe kuwa unastahili heshima na haki yako ya ndoa. Asipojirekebisha basi ndoa yenu haitakuwa na maana.