Habari Mseto

Wabakaji kuadhibiwa kitamaduni, aonya Otichilo

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

GAVANA wa Kaunti ya Vihiga Wilbur Otichilo ameonya kuwa wahalifu wa dhuluma za kingono wanaonajisi watoto na kubaka wanawake watakabiliwa kwa mujibu wa tamaduni za jadi za jamii ya Wanyore.

Dkt Otichilo alisema kutokana na ongezeko la dhuluma za kingono dhidi ya watoto na akina mama, wazee katika jamii hiyo hawatakuwa na budi ila kutumia mila za tangu jadi kukabiliana na wahalifu husika.

Akihutubu wakati wa sherehe za tamaduni za jamii hiyo katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Ebusakami iliyoko kaunti ndogo ya Luanda, Dkt Otichilo alisema adhabu ya kitamaduni ilikuwa kali kuliko sheria ya kisasa.

Kwa muujibu wa mila hizo ni kwamba iwapo mtu atahusika katika unajisi au ubakaji, atalishwa chakula fulani wakati wa sherehe na ikiwa ana hatia huenda akafariki papo hapo kwani ni mwiko kwa mtu kama huyo kushiriki vyakula fulani katika jamii.

Gavana Otichilo alisema eneo hilo linaendelea kushuhudia ongezeko la visa vya dhuluma za kimapenzi na kingono dhidi ya akina mama na watoto.

“Kuna baadhi ya tamaduni ambazo tumeacha licha ya umuhimu wake wa kimaadili katika jamii kama vile kufanya matambiko na kushiriki chakula fulani kwa watu ambao ni washukiwa wa uhalifu wa kingono,” alisema Dkt Otichilo.

Dkt Otichilo alisema awali desturi hiyo ilikuwa inaogepewa na hivyo visa vya dhuluma za kingono vilikuwa vimekabiliwa.

Gavana huyo aliongeza kuwa wanamuziki kutoka katika jamii hiyo watadhaminiwa na kaunti kutunga nyimbo za kukejeli na kuwaanika washukiwa wa unajisi na ubakaji ili wajulikane katika jamii.

“Tutashirikiana na wanamuziki wetu kubuni nyimbo za kuwaanika na kuwakejeli wanaume wanaonajisi watoto na kubaka akina mama ili wajulikane katika jamii na kutengwa,” alisema.

Naye Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Vihiga Bi Beatrice Adagala alilamikia ongezeko la unajisi wa watoto unaofanywa na watu wa familia zao.

Bi Adagala alisema iwapo tamaduni za jadi zitachangia kukabiliana na tatizo hilo, bila shaka atauunga mkono mkondo huo.

“Tumechoka kushuhudia ongezeko la visa vya kunajisi watoto haswa na watu wa familia zao. Tuko tayari kuunga kila mbinu ikiwa ni pamoja na desturi kumaliza uhalifu huu,” alisema Bi Adagala.

Bi Adagala aliwataka wanaume kuheshimu maadili na kuachana na tabia ya kunajisi watoto na kubaka wanawake.