Habari Mseto

Mahakama yampa idhini Timothy Njoya kumtimua 'mama yake'

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA ya Nyeri imemkubalia Kasisi Mstaafu  wa kanisa la PCEA Timothy Njoya kumtimua ‘mama yake wa kambo’ kutoka kwa ardhi ya ekari nne iliyomilikiwa na mwendazake babaye eneo la Mukurweini.

Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo Philip Mutua alidinda kumtaja Bi Mary Wangui Maina kama mmiliki wa ardhi hiyo na badala yake kusema kuwa yeye ni mtu aliyeivamia kinyume cha sheria.

Bw Mutua alisema Bi Maina anafaa kuondoka kwa ardhi hiyo kwa hiari, ambayo imesajiliwa kama LR No.Muhitu/Thiha/324, katika kipindi cha siku 30.

Iwapo atakosa kufanya hivyo, basi mahakama itatoa agizo la kumfurusha na atatakiwa kugharamia gharama zote za kumtimua.

Bw Njoya pamoja na Bi Maina wamekuwa wakizozania umiliki wa ardhi hiyo mahakamani tangu mwaka 2005.

Mahakama pia ilimtuza kasisi huyo Sh100,000 kama fidia ya ardhi yake kuvamiwa.

“Mtu yeyote aliyenyang’anywa ardhi ana haki ya kuitwaa tena na kufidiwa kwa matatizo aliyopata,” akasema hakimu Mutua na kumtaka Bi Maina kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Kupitia kwa Shirikishola Mawakili Wanawake nchini (Fida), Bi Maina alisisitiza kuwa alikuwa mke halali wa babaye kasisi Njoya, Nahashon Njoya Murere kwa miaka 19 kuanzia 1977 hadi Januari 2, 1996.

Aliwasilisha stakabadhi ya Wazee wa kijiji cha Ngoru, kata ya Muhito kuthibitisha kuwa yeye na mwendazake walikuwa wanandoa.

“Mnamo Februari 5, 1977, marehemu alifika kwa wazazi wangu Nyeri na kuwaambia alikuwa na nia ya kunioa,” akasema.

Alisimulia kuwa kabla ya ‘mumewe’ kufariki, walikuwa wanaishi pamoja katika ardhi hiyo yenye mzozo, ambayo anaitambua kama nyumbani kwake.

“Tulipata watoto wanne pamoja; George Mathenge Njoya, Anthony Maingi Njoya, Nelius Muthoni Njoya na Lesho Njoki Njoya. Ardhi hii ni sehemu ya mali ya mume wangu ambaye pia ni babaye mlalamishi,” akasema.