Dereva wa tuk-tuk atekwa nyara Nyali
NA FARHIYA HUSSEIN
USIKU wa Jumatano, kijana Amin Mohammed Alawi, 28, alitembelea mmojawapo wa mikahawa ya Nyali, Mombasa kama ilivyokuwa desturi yake akiwa na baadhi ya marafiki zake.
Lakini jioni hiyo, kijana huyo hakurejea nyumbani, jambo lililofanya familia yake kuanza kufanya msako mkubwa katika maeneo yote ambayo walidhani anaweza kupatikana huko.
Licha ya juhudi zao, hawajafanikiwa kumpata.
“Alikuwa nje na marafiki zake watano ambapo walitokea watu sita waliokuwa wamejitambulisha kama maafisa wa polisi waliwaamuru wakae chini. Walikuwa na silaha na walikuwa wamevalia kiraia. Basi wakaamuru ndugu yangu na marafiki zake kila mmoja ataje nambari zake za simu za mitandao ya Airtel na Safaricom. Ni kama vile walitaka kuwa na uhakika na waliyetaka kumteka nyara,” alielezea Bw Ahmed Mohamed, ambaye ni kaka mkubwa wa Bw Amin.
Familia inaripoti kwamba kijana huyo alinyakuliwa kwa nguvu na kutupwa ndani ya gari aina ya Probox ya kijivu.
“Ndugu yangu hajawahi kumkosea yeyote. Inaogopesha kwamba siku moja anatoka nyumbani na kutoweka ghafla,” akasikitika Bw Ahmed.
Diwani wa Old Town Abdirahman Hussein amelaani kitendo cha watekaji nyara hao.
“Tunaomba maafisa wa usalama kufanya kila wawezalo kuhakikisha wanatambua aliko. Hii ni nchi ya sheria, ikiwa mtu ana makosa lazima akamatwe, apelekwe katika kituo cha polisi na kisha kufikishwa mahakamani. Hatutaki kufanya dhana bali tunauliza maswali muhimu na tunatumai atapatikana,” akasema Bw Hussein.
Familia inasema Bw Amin alifanya kazi kama dereva wa Tuk-tuk tangu alipokuwa na umri wa miaka 20.
“Alizaliwa Mogadishu, Somalia na tukahamia Kenya mwaka 2011 kama wakimbizi. Alisomea masuala ya kidini kwenye madrassa na kisha akaanza kufanya kazi kama dereva wa tuk-tuk alipokuwa na umri wa miaka 20,” aliongeza Bw Ahmed akisisitiza ndugu yake mdogo hana kesi zozote zilizopo na hajawahi kukamatwa awali.
Familia hiyo tayari imeripoti suala hilo katika kituo cha polisi cha Nyali chini ya nambari ya matukio OB 23/4/1/2024.
“Ikiwa ana kesi yoyote, walifaa kumpeleka kituoni na kisha mahakamani. Tunahangaika na hatujapumzika tangu apotee. Huyu ni mtu wa kawaida tu aliyekuwa tegemeo kwa familia yake,” alisema babake kijana huyo.
Alihimiza serikali kuingilia kati na kuwasaidia kumtafuta.
“Tumekwenda katika vituo vyote vya polisi hapa lakini hatujampata,” alisema mzazi huyo.
Mama yake, Bi Aisha Adew Noor, ambaye alikuwa akitiririkwa na machozi, hakuwa na mengi ya kusema isipokuwa kuomba mtoto wao wa tatu kurudishwa.
Afisa wa Masuala ya Dharura katika shirika la Haki Africa Mathias Shipeta alisema hiyo ni kesi ya kwanza waliyopokea mwaka 2024.
“Tunahofia nyingine zinaweza kurekodiwa na ndiyo maana tunahimiza kesi kama hii ipewe kipaumbele. Ikiwa hatorejea ndani ya wiki, tutakuenda mahakamani. Hatunyooshi kidole cha lawama kwa serikali bali tunatafuta jinsi Bw Amin anavyoweza kupatikana,” akasema Bw Shipeta.
Bw Shipeta aliomba uchunguzi wa haraka kufanyika.
Familia inataka rekodi za kamera za CCTV zitolewe zikionyesha Bw Amin katika dakika zake za mwisho kabla ya kutoweka, ikisema zitasaidia pakubwa.