Makala

Wataka ujenzi wa barabara sehemu zenye mashambulio ya Al Shabaab

December 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

MADEREVA na wasafiri wanaotumia barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen wanamtaka mwanakadarasi wa ujenzi wa barabara hiyo kuanza ujenzi huo kwenye sehemu ambazo zinatambulika kuwa kero kwa mashambulizi ya Al-Shabaab.

Wasafiri na madereva hao wameonekana kukerwa na mwanakandarasi huyo anayedaiwa kuendeleza ujenzi wa barabara kwenye sehemu ambazo hazijashuhudia changamoto yoyote ya usalama.

Ujenzi wa barabara ya Lamu kuelekea Garsen ambao ulianzishwa rasmi mapema mwaka huu unatekelezwa kuanzia eneo la Gamba na Witu na kufikia sasa tayari barabara hiyo imekamilika kwa takriban asilimia 20.

Katika mahojiano na wanahabari Jumatatu, watumiaji hao wa barabara walisema ni bora mwanakandarasi huyo kuanzisha ujenzi hasa kwenye maeneo ya Milihoi, Mambo Sasa, Lango la Simba na Nyongoro kabla ya kukamilisha ujenzi wake kwenye maeneo salama.

Ujenzi wa barabara ya Lamu hadi Garsen unatekelezwa na kampuni ya H-Young na unatarajiwa kukamilika kufikia Disemba 31, 2019.

Bw Peter Kariuki ambaye ni mmoja wa madereva kwenye barabara hiyo ya Lamu hadi Garsen alisema sehemu kama vile Milihoi, Mambo Sasa, Lango la Simba na Nyongoro ziko hali duni, jambo ambalo anadai limetoa mwanya rahisi kwa Al-Shabaab kuvamia magari ya usafiri na pia yale ya walinda usalama.

Barabara ya Lamu kuelekea Garsen. Wasafiri na madereva wanaotumia barabara hiyo wamemtaka mwanakandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo kuanza ujenzi hasa kwenye sehemu ambazi zimekuwa zikilengwa na Al-Shabaab. Picha/ Kalume Kazungu

“Sioni sababu ya mwanakandarasi kuanzisha ujenzi wa barabara yetu kwenye maeneo salama. Ni heri aanze ujenzi kwenye sehemu hatari, ikiwemo Milihoi, Nyongoro, Mambo Sasa, Lango la Simba na kwingineko ambako Al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi. Tunaamini barabara ikiwa shwari hasa kwenye sehemu hizo, huu uvamizi hautakuwepo tena,” akasema Bw Swaleh.

Bw Bakari Said ambaye ni mmoja wasafiri kwenye barabara hiyo aliipongeza serikali kwa kuanzisha kambi za polisi na jeshi kwenye sehemu hizo hatari.

Bw Bakari aidha alisema utovu wa usalama utazikwa kwenye kaburi la sahau katika sehemu hizo iwapo barabara pia itajengwa na kutiwa lami ili magaidi wakose mahali pa kutega vilipuzi vyao.

“Ikiwa barabara itajengwa na kutiwa lami hasa kwenye sehemu hatari, basi hao magaidi watakosa pa kuweka hivyo vilipuzi vyao. Hii itamaanisha usalama utaboreka zaidi ikizingatiwa kuwa sehemu hizo tayari kuna kambi za walinda usalama zimebuniwa,” akasema Bw Bakari.

Mojawapo ya sehe,mu ya barabara ya Lamu-Gasen ambayo ujenzi wake umekamilika eneo la Gamba-Witu. Picha/ Kalume Kazungu

Bi Aisha Yusuf aidha aliziomba kampuni za mawasiliano nchini kuhakikisha wanajenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo hayo ili iwe rahisi kwa wakazi kupiga ripoti punde wanapowaona wahalifu.

“Mawasiliano hakuna kwenye maeneo husika. Ombi langu kwa kampuni za mawasiliano ni kwamba huku serikali ikijenga barabara pia wafikirie kujenga minara ya mawasiliano ili iwe rahisi kwetu kuwasiliana na wahusika iwapo uvamizi utafanyika kwenye maeneo husika,” akasema Bi Yusuf.

Mradi huo wa barabara ambao ni umbali wa kilomita 135 umekadiriwa kugharimu serikali kuu kima cha Sh 10.8 bilioni.