Wachuuzi wa mafuta ya kupika wanavyohadaa watu kwa vibuyu vyenye maji
NA RICHARD MAOSI
WAKAZI wa Kitengela, Kaunti ya Kajiado wametakiwa kuwa macho ili kuepuka mtego wa matapeli, wanaowauzia maji badala ya mafuta ya kupikia.
Wahuni wamekuwa wakipakia lita 1, 2, tano, 10 na hata 20 za mafuta, huku baadhi ya vibuyu vikiwa vimejazwa maji ambayo husambazwa kwenye mikahawa na makazi ya watu.
Kwa sababu ya mfumuko wa bei ya bidhaa, wanunuzi kwa upande mwingine wamekuwa waking’ang’ania mafuta hayo ambayo huuzwa kwa bei rahisi, lakini wanapofika nyumbani hupata ni maji.
Ni jambo ambalo limezua hisia mseto mitandaoni, wengi wakishauriwa kununua bidhaa zao kwenye maduka ya kijumla badala ya kutumia njia ya mkato.
“Watu waende dukani badala ya kununua vichochoroni,” akashauri Esborn Wasilwa.
Baadhi ya wakazi Kajiado pia wamekiri kwamba biashara hii imekuwa ikiendeshwa mtaani Rongai, ila matapeli walihamia Kitengela na Mlolongo baada ya njama zao kugunduliwa.
Bi Anne Mbeyu mchuuzi wa chapati, samosa na maandazi mjini Kitengela anasema aliuziwa maji msimu Krismasi 2023.
Anadai sio yeye tu, wanaoadhirika zaidi wakiwa ni akina mama ambao huuza vyakula na kundi jingine likiwa la wamiliki wa mikahawa ambao wanategemea mafuta ya kupikia kuendesha shughuli za kila siku.
Wengi wao hushawishika kununua mafuta yanayouzwa mitaani kwa sababu ni nafuu na lita moja inachuuzwa kati ya Sh20 hadi Sh150.
“Hii inaashiria kwamba mnunuzi anaweza kuokoa karibu na Sh100 kwa kila lita ya mafuta ambayo hununua.
Kinyume na bei halisi ya sokoni ambayo kwa kawaida huwa ni kati ya Sh220 na 240 kwa lita,” anasema.
Anasema huenda hali ngumu ya uchumi ndio imewasukuma vijana wengi mtaani kubuni njia ambayo sio halali wakati wa kuzumbua riziki.
Hata hivyo, Shirika la Kukadiria Viwango Vya Bidhaa Kenya (KEBS), miezi kadhaa iliyopita lilibaini kwamba baadhi ya mafuta yanayoingizwa humu nchini hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Hii ina maana kwamba Wakenya wanakabiliwa na hatari ya kutumia mafuta ambayo yamechafuliwa.